Saturday, September 1, 2012

WENGER ALIYEENDA KULALA MAPEMA WAKATI WENZAKE WANAKESHA KUSAJILI, ACHIMBA MKWARA... TUTAWASHANGAZA MSIMU HUU...


KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema ameshazoea timu yake kudharauliwa na kutopewa nafasi yoyote ya kufanya vizuri mwanzoni mwa msimu.

Kutosajili nyota wapya katika siku za mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili kumeamsha mijadala kwamba huenda hatimaye huu ndio msimu ambao kikosi cha Wenger kitatupwa nje ya Top 4.

Hata hivyo, Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 62 amepuuza mitazamo hiyo, akikumbushia namna Arsenal ilivyomaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita wa Ligi Kuu ya England baada ya wengi kubashiri mabaya kwa Arsenal.

"Hamjawahi kutarajia makubwa kutoka kwetu, lakini daima tunao uwezo wa kuwashangaza," alisema.

"Niliposikiliza utabiri uliotolewa siku kama hii mwaka jana, ilibashiriwa kwamba tungemaliza katika nafasi ya 10 ama ya 15. Tukamaliza wa tatu."

Wenger ameituhumu jamii "kuendeshwa kwa hisia' ambayo soka linafanyakazi humo na kusababisha kauli kali kutoka kwa mashabiki na vyombo vya habari.

"Kuna kauli kali kutoka kwenye Twitter, radio na internet. Hiyo inakuonyesha namna ambavyo jamii ya kisasa ilivyo na hisia," Wenger aliendelea.

"Jamii imesogea kutoka kuwa mbali na matukio na kuwa yenye hisia kali.

"Tumehama kutoka katika jamii inayotafakari na kuwa jamii inayoendeshwa na hisia.

"Nadhani ni vyema kufikiri kabla hujasema jambo. Ni rahisi sana kusema."

Arsenal ambayo itasafiri kwenda kucheza ugenini dhidi ya Liverpool kesho Jumapili, bado inasaka ushindi wake wa kwanza na goli lake la kwanza tangu ilipomuuza mfungaji bora wa ligi kuu ya England wa msimu uliopita Robin van Persie kwa mahasimu wao Manchester United, na Wenger anaamini Brendan Rodgers naye yuko katika presha kama yake.

Aliongeza: "Kuna matarajio makubwa sana kwa Liverpool. Naamini Liverpool ni timu nzuri.

"Nikiwa nimeshuhudia mechi zote nilizoshuhudia hadi sasa katika Ligi Kuu ya England, ni vigumu kuchagua timu moja kuwa ndiyo ngumu zaidi ya nyingine.

"Liverpool wana nafasi ya kupigania kupanda juu, lakini sisi tunachuana na Chelsea, Manchester City na Manchester United sasa pia."

Mashabiki wa Arsenal ambao "wamesahau" kubeba makombe kwa miaka 7 wamekuwa wakimshambulia vikali Wenger kwa kutozungumzia mipango na dhamira ya klabu hiyo kuja kutwaa makombe na badala yake kuzungumzia timu kuongezeka ubora tu.

No comments:

Post a Comment