Tuesday, September 18, 2012

WENGER AHOFIA THEO WALCOTT KUTIMKA ARSENAL


Straika Theo Walcott
LONDON, England

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger ameelezea hofu yake kuhusiana na mkataba mpya wa Theo Walcott na kusema kwamba kuna hatari winga huyo akaondoka klabuni hapo.


Straika huyo wa kimataifa wa England alipokewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa klabu yake kwenye Uwanja wa Emirates wakati alipoingia uwanjani na kufunga wakati Arsenal ikishinda 6-1 dhidi ya Southampton katika mechi yao ya Ligi Kuu ya England mwishoni mwa wiki.


Hali hiyo ilitokana na uvumi uliotanda kuelekea mwishoni mwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi kwamba  Walcott amekataa ofa ya mkataba mpya, yenye mshahara wa paundi za England 75,000 kwa wiki (Sh. Milioni 190) na badala yake alitaka alipwe mshahara wa paundi za England 100,000 (Sh. Milioni 250).


Na kwavile straika huyo mwenye miaka 23 sasa anaingia katika mwaka wa mwisho wa kutumikia mkataba wake, Wenger anaweza kushuhudia nyota mwingine mwenye jina kubwa akiondoka katika klabu yake, ambayo tayari msimu huu imewapoteza Robin van Persie aliyehamia Man U na Alex Song aliyetua Barcelona.


Ameliambia gazeti la Guardian: “Hivi sasa, bado natumai kwamba tutaongeza mkataba wake, hivi sasa hilo halinisumbui.


“Ni wazi kwamba itafikia hatua… ikiwa, hadi April, bado hajasaini, hapo sasa unaweza kufikiri kwamba jambo hilo litakuwa gumu."

No comments:

Post a Comment