Saturday, September 1, 2012

SOMA ALICHOSEMA BERBATOV BAADA YA KUJIUNGA FULHAM KWA MKATABA WA MIAKA MIWILI... FIORENTINA WALIMKATIA TIKETI YA NDEGE HAKWENDA, WAKASEMA BORA HAKUJA

Berbatov akishikilia jezi ya klabu yake mpya ya Fulham baada ya kutambulishwa

STRAIKA wa Manchester United, Dimitar Berbatov amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea klabu ya Fulham.

Nyota huyo wa Bulgarian, 31, alikuwa akitakiwa na klabu kadhaa, zikiwamo za Italia za Fiorentina na Juventus, lakini akachagua kubaki katika Ligi kuu ya England.

Fulham wamekataa kutaja kiasi walicholipa ili kumpata straika huyo.

"Haraka sana niliposikia kwamba Fulham wananihitaji, maamuzi yangu ya kujiunga nao yalikuwa ni mepesi mno," alisema Berbatov, ambaye alipata kucheza chini ya kocha wa Fulham, Martin Jol wakati wakiwa pamoja Spurs.

"Nimevutiwa na mipango ya hapa na watu wamenifanya nijione nakaribishwa. Kuna hisia na ukaribu klabuni hapa na nashindwa kusubiri kuanza kuitumikia."

Jol aliongeza: "Dimitar ni mchezaji ambaye daima nimekuwa nikimkubali. Ni mchezaji mwenye ubora wa juu na ni 'fundi' hasa ambaye atatupa safu ya ushambuliaji ambayo tulikuwa tukiihitaji. Anapokuwa hafungi magoli, ubunifu wake umekuwa ukipika magoli kwa wachezaji wenzake."

Fiorentina walidhani kwamba wameshamnasa Berbatov. Walidai kwamba wamepewa ruhusa na United ya kuzungumza naye lakini hakwenda mjini Florence kwa ajili ya mazungumzo wakati wakiwa tayari walishamlipia tiketi ya ndege.

"Tunafuraha kwamba hakuja Fiorentina," taarifa ya klabu hiyo ya Italia ilisema. "Hastahili kuwa kwenye jiji letu, hastahili kuvaa jezi yetu na hastahili thamani yetu." 

No comments:

Post a Comment