Thursday, September 6, 2012

SIMBA YACHAKAZWA 3-0 NA SOFAPAKA YA KENYA LEO ... BEKI MPYA KUTOKA MALI ASABABISHA PENATI, MGHANA AKUFFOR AUMIA ... OCHIENG, KINJE, NGASSA, BOBAN HOI

Straika Daniel Akuffor wa Simba (kulia) akipiga shuti kuelekea lango la Sofapaka wakati wa mechi yao ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.
Taratibu... Straika Akuffor akitolewa uwanjani baada ya kuumizwa na beki Antony Kimani wa Sifapaka wakati wa mechi yao ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. 
Mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba wamejikuta wakiendeshwa puta na kupata kipigo kisichotarajiwa cha mabao 3-0 kutoka kwa Sofapaka inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya katika mechi yao ya kimataifa ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Washindi walipata bao la utangulizi katika dakika ya 18 kwa njia ya penati baada ya beki mpya wa kimataifa wa Simba, raia wa Mali
Komalmbil Keita kucheza faulo katika eneo la boksi na mshambualiaji wa zamani wa Yanga, John Baraza akatumbukiza mpira wavuni kwa shuti lililomshinda kipa Juma Kaseja.

Safu ya mabeki wa Simba iliendelea kuwapa hofu mashabiki wa klabu yao baada ya Pascal Ochieng na Keita kushindwa kuwasiliana na Kaseja aliyekuwa akitoka kujaribu kumzuia mfungaji bila ya mafanikio na kuwapa wageni bao la pili katika dakika ya 57 kupitia tena kwa Baraza.

Kikosi cha Simba kinachonolewa na Mserbia Milovan Cirkovic kiliwasononesha mashabiki wao waliofika i kuwashangilia baada ya mabeki wake kuruhusu bao la tatu katika dakika ya 66 kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na mchezaji wa zamani wa Azam, Osborne Monday kumaliziwa vyema  fuatia shuti la Joseph Nyaga aliyemalizia vyema kazi nzuri iliyofanywa na mchezaji wa zamani wa klabu ya Azam, Osborne Monday.

Safu ya kiungo iliyotarajiwa kuwa 'kali' ya Salim Kinje na Mwinyi Kazimoto ilishindwa kuonyesha makali mbele ya Sofapaka, kama ilivyokuwa kwa viungo-washambuliaji Haruna Moshi 'Boban', Mrisho Ngassa aliyetua kwa kishindo katika timu hiyo akitokea Azam na mshambuliaji wao Christopher Edward aliyeibuka kinara wa kupachika mabao katika michuano iliyomalizika hivi karibuni ya Ligi ya Super8 na kuisaidia Simba B kutwaa ubingwa.

Awali, katika dakika ya 35, Simba walipata pigo baada ya Straika wao tegemeo kwa sasa, Mghana Akuffor kuumia vibaya baada ya kupigwa kiwiko kwenye chembe cha moyo na mchezaji wa Sofapaka, Antony Kimani. 


Alianguka uwanjani na akawa akipaparika kama mtu mwenye kifafa kabla ya kupoteza fahamu, ambapo daktari wa Simba, Cosmas Kapinga alisema hali hiyo ilitokana na kushindwa kupumua baada ya ulimi wake kugeukia ndani na kuziba njia ya hewa.

Mpira ulisimama kwa dakika tano wakati akitibiwa na alipozinduka alitaka kuendelea kucheza lakini daktari Kapinga alimkataza na hivyo akatolewa uwanjani. 

Kipigo cha leo kimemuacha kocha Milovan katika wakati mgumu wa kukiboresha kikosi chake kwani zimebaki siku chache kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Azam Jumanne katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kuivaa Sofapaka leo, Milovan aliahidi soka safi na kusema kwamba mechi hiyo ndio kipimo chao kabla ya kucheza dhidi ya Azam kwani wameshajifua vya kutosha, hasa walipokuwa katika kambi yao jijini Arusha.

Licha ya ubutu wa safu yao ya ushambuliaji, rekodi ya mabeki wa Simba pia haionyeshi kuwa wako 'ngangari' vya kutosha tangu aondoke Kevin Yondan aliyejiunga na Yanga, kwani penati waliyoruhusu leo dhidi ya Sofapaka ni ya pili katika mechi zao nne za  kirafiki za hivi karibuni. 


Penati nyingine ilishasababishwa na Pascal Ochieng. Mabeki hao vilevile wana rekodi nyingine 'mbovu' ya kujifunga mara mbili katika mechi hizo nne za kujipima nguvu, 'wadunguaji' wa mabao hayo ya langoni kwao wenyewe wakiwa ni mabeki Juma Nyosso na Keita.Rekodi katika mechi hizo zinaonyesha kuwa beki Ochieng aliyeondoka AFC Leopards ya Kenya kutokana na kukosa namba katika kikosi cha kwanza, alisababisha penalti moja wakati Keita ambaye ametua kutoka Mali, amejifunga goli moja na kusababisha penati moja huku Nyosso naye akijifunga moja katika mechi hizo nne ambazo Simba waliwafunga JKT Oljoro 2-1, wakawabwaga Mathare United 2-1 pia na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Sony Sugar ya Kenya.   

Akuffor ndiye ambaye ameonekana kuwa mchezaji 'jembe' baada ya kufunga katika mechi zote tatu za kwanza kabla ya leo kuumia.

VIKOSI
Simba: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah/ Said Nasoro 'Chollo', Pascal Ochieng/ Juma Nyosso (dk.75), Komalmbil Keita
/ Paul Ngalema (dk.75), Mwinyi Kazimoto, Salim Kinje/Ramadhani Chombo 'Redondo' (dk.46), Haruna Moshi ‘Boban’, Edward Christopher/ Kigi Makasi (dk.75), Daniel Akuffor/ Abdalla Juma (dk.40) na Mrisho Ngassa.
 

Sofapaka: Duncan Ochieng, Antony Kimani, James Situma, Edgar Ochieng, George Owino, Collins Okoti, Osborne Monday, Humphrey Mieno, Kago Danson, Joseph Nyaga na John Baraza.

No comments:

Post a Comment