Wednesday, September 26, 2012

PIGO JINGINE MAN UTD...VALENCIA NAYE AUMIA, ATEMBELEA MAGONGO

Antonio Valencia
Tukio ambalo Valencia anasemekana aliumia wakati wa mechi yao dhidi ya Liverpool Jumapili

MANCHESTER United wamepata pigo jingine mbali na nahodha Nemanja Vidic kuonekana kwamba atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nane kutokana na upasuaji wa goti.

Winga Antonio Valencia aliondoka kwenye uwanja wa mazoezi wa Man U akitembelea magongo.

Mguu wa kulia wa Valencia ulikuwa umevishwa kiatu maalum wakati madaktari wa Man U wakiendelea kuchunguza ukubwa wa majeraha aliyoyapata wakati waliposhinda 2-1 dhidi ya Liverpool Jumapili.

Winga huyo aliumia wakati alipopata penalti ambayo iliamua matokeo ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa Anfield, licha ya kwamba beki wa Liverpool, Glen Johnson alimtuhumu kwamba alijiangusha.

Kukosekana kwa Vidic kunaifanya Man U ikibakiwa na mabeki wa kati wawili tu Rio Ferdinand na Jonny Evans, wakati Chris Smalling na Phil Jones wanaendelea kuuguza majeraha ya upasuaji waliofanyiwa. Pia imeamsha maswali kuhusu hali ya goti la kulia la Vidic, kwani ndilo hilo hilo aliloumia beki huyo mwenye umri wa miaka 30 wakati wa mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya FC Basel Desemba mwaka jana na kumuweka nje ya uwanja kwa miezi tisa.

Taarifa ya klabu ilisomeka: "Nemanja Vidic amefanyiwa upasuaji wa goti la kulia na atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha kufikia wiki nane. Sir Alex, alichukua hatua za tahadhari, akampumzisha Vidic wikiendi, baada ya kulalamikia goti lake kuvuta."

Vidic sasa atakosa mechi tano za zilizobaki za Man U katika hatua ya makundi ya Ligi ya Klabu Bingwa na mechi nane za Ligi Kuu ya England.

Smalling na Jones wanatarajiwa kurejea ndani ya wiki sita zijazo hivyo kwa sasa Ferguson ni lazima awategemee Evans, ambaye amecheza mechi tatu tangu alipotoka kufanyiwa upasuaji wa mguu, huku akihakikisha hampi mzigo mkubwa Ferdinand ili asitoneshe majeraha yake ya muda mrefu ya mgongo.

No comments:

Post a Comment