Thursday, September 20, 2012

MESSI AZIDI KUMBURUZA CRISTIANO RONALDO

Straika wa Barcelona, Lionel Messi akipiga mpira wakati wa mechi yao ya Kundi G la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Spartak Moscow kwenye Uwanja wa Nou Camp mjini Barcelona, jana usiku Septemba 19, 2012. Picha: REUTERS


Straika wa Barcelona, Lionel Messi akipongezwa na mchezaji mwenzake David Villa baada ya kufunga goli la ushindi wakati wa mechi yao ya Kundi G la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Spartak Moscow kwenye Uwanja wa Nou Camp mjini Barcelona, jana usiku Septemba 19, 2012. Picha: REUTERS
Cristiano Ronaldo akishangilia kwa kuteleza kwa magoti baada ya kufunga goli la ushindi dhidi ya Manchester City katika mechi yao ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid juzi. Real ilishinda 3-2.

BARCELONA, Hispania
LIONEL Messi amethibitisha kwamba kila linalofanywa na Cristiano Ronaldo yeye anaweza kulifanya vizuri zaidi wakati alipofunga mara mbili kwa Barcelona na kuiokoa timu yake kwenye ushindi wa kutokea nyuma wa 3-2 nyumbani dhidi ya Spartak Moscow katika mechi yao ya ufunguzi wa Kundi G la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya jana usiku.


Ronaldo, anayewania kuhitimisha utawala wa Messi wa kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia kwa miaka mitatu mfululizo, aliulipua kwa shangwe uwanja wa Bernabeu wakati alipofunga goli katika dakika ya 90 lililowapa Real Madrid ushindi 3-2 dhidi ya Manchester City katika Kundi D Jumanne.


Messi si tu kwamba alifunga goli la kusawazisha la Barca katika dakika ya 71 dhidi ya timu hiyo ya Urusi isiyopewa nafasi kwenye Uwanja wa Nou Camp, bali pia alifunga goli la ushindi kwa kichwa ambacho ni adimu kwake kutokana na kuwa mfupi dakika 10 kabla ya mechi kumalizika.


Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina amekuwa mfungaji bora wa michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Ulaya kwa misimu minne mfululizo iliyopita na mabao yake mawili ya jana yamemfanya kufikisha jumla ya magoli 53 katika mechi 69 za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wakati Ronaldo amefunga magoli 39 katika mechi 81.


"Tulistahili kushinda lakini ilikuwa mechi ngumu sana," Messi aliiambia televisheni ya Hispania.


"Sio rahisi wanapojilinda kwa kukaa nyuma sana na unashindwa kupata nafasi," aliongeza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka  25, ambaye sasa amefunga jumla ya magoli 109 katika mechi 100 za michuano zilizopita kwa Barca.


"Walikuwa wanajilinda kwa kujiamini katika eneo lao la penalti na walikuwa na washambuliaji wenye kasi na nguvu ambao wanaweza kupanda mbele haraka.


"Mambo yalianza kuwa magumu lakini tuliendelea kushambulia na kufanikiwa kugeuza mambo."

No comments:

Post a Comment