Wednesday, September 26, 2012

MANCHESTER CITY WAAGA KOMBE LA CARLING KWA KUSHINDILIWA MABAO 4-2, CHELSEA YAUA 6-0 HUKU EVERTON NA WEST HAM NAZO ZIKICHEZEA VICHAPO

Mario Balotelli wa Manchester City akifunga goli la kwanza wakati wa mechi yao ya raundi ya tatu ya Kombe la Carling dhidi ya Aston Villa kwenye Uwanja wa Etihad mjini Manchester, jana Septemba 25, 2012. (Picha: Reuters)
Safi mwana...! Carloz Tevez (katikati) akimpongeza Balotelli baada ya kufunga goli la kwanza.
Victor Moses wa Chelsea (wa pili kushoto) akishangilia na wachezaji wenzake baada ya kufunga goli la sita dhidi ya Wolves wakati wa mechi yao ya raundi ya tatu ya Kombe la Capital One (zamani Kombe la Carling) dhidi ya Wolves kwenye Uwanja wa Stamford Bridge jana, Septemba 25, 2012. (Picha: Reuters)
LONDON, England
MABINGWA wa Ligi Kuu ya England,  Manchester City na klabu iliyo katika kiwango chake cha juu hivi sasa ya Everton, wote wamefungashwa virago mapema katika Kombe la Carling jana usiku, huku makocha wao wakistahili kubeba lawama baada ya kubadili vikosi vyao vyote katika mechi hizo zilizokuwa za raundi ya tatu.

Man City walichapwa 4-2 baada ya dakika za nyongeza mbele ya wapinzani wao katika Ligi Kuu, Aston Villa baada ya mabingwa hao wa England kuwaacha nje wachezaji wote waliocheza dhidi ya Arsenal Jumapili, wakati Everton waliowapumzisha nyota wao sita wakichapwa 2-1 katika mechi yao dhidi ya timu ya daraja la kwanza ya Leeds United.

Chelsea pia walifanya mabadiliko kadhaa lakini walitinga raundi ya nne baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Wolverhampton Wanderers kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

Mario Balotelli aliwafungia Man City goli la utangulizi kwa shuti la chini lililokwenda wavuni na kuwa na la kwanza pia kwake kuifungia klabu tangu Machi, kabla Villa hawajasawasisha baada ya kiungo Gareth Barry kujifunga.

Aleksandar Kolarov alipiga 'fri-kiki' kali iliyoipa Man City uongozi tena katika dakika ya 64, lakini Gabriel Agbonlahor wa Villa  akasawazisha bao hilo dakika tano baadaye na hivyo kusababisha sare iliyolazimisha mechi hiyo kuongezewa dakika 30.

Charles N'Zogbia aliipa Villa uongozi wa 3-2 baada ya kuuwahi mpira uliokuwa ukizagaa karibu na lango la Man City na kupiga shuti lililokwenda wavuni kabla Agbonlahor hajafunga la nne baada ya shuti lake kubabatizwa na kumpita kipa wa Man City, Costel Pantilimon.

Everton, wanaokamata nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, walitanguliwa katika dakika ya nne tu wakati  Aidy White alipowatoka mabeki wao na kupiga shuti lililokwenda wavuni.

Leeds walipata bao la pili wakati shuti la Danny Pugh liliposindikizwa wavuni na Rodolph Austin katika kipindi cha pili kabla Sylvain Distin hajaifungia Everton goli la kufutia machozi kuelekea mwishoni mwa mechi.

Garry Monk aliifungia Swansea City katika dakika ya 90 na kuipa ushindi wa 3-2 dhidi ya timu ya daraja la pili ya Crawley, huku Wigan Athletic wakishinda ugenini 4-1 dhidi ya wapinzani wao katika Ligi Kuu ya England, West Ham United.

No comments:

Post a Comment