Wednesday, September 19, 2012

KLABU LIGI KUU, WADHAMINI VODACOM KUTETA

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Rene Meza (kushoto) akimfafanulia jinsi mkataba wa udhamini wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara ulivyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi , Said Mohammed, wakati wa hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia wa pili kutoka kushoto ni Makamu wa Pili wa Rais wa TFF,  Nasibu Nyamlani na Ofisa Mkuu wa Masuala ya  Sheria wa Vodacom, Wallarick Nittu.

KLABU za Ligi Kuu ya Vodacom zimekubaliana kukutana na mdhamini (kampuni ya huduma za simu ya Vodacom) kuzungumzia kipengele cha mkataba wa ligi hiyo kinachozuia kampuni nyingine za mawasiliano kudhamini timu zinazocheza Ligi Kuu.

Maazimio hayo yalifikiwa jana (Septemba 18 mwaka huu) katika kikao kati ya klabu hizo na Kamati ya Ligi kilichofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wallace Karia.

Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.

Maazimio mengine ya kikao hicho ni TFF kuiandikia barua African Lyon ambayo itaipeleka kwa mdhamini wake (Zantel) ikielezea hatua hiyo ili kusimamisha udhamini huo wakati ikisubiri matokeo ya mazungumzo kati ya klabu hizo na mdhamini wa Ligi Kuu juu ya kipengele cha kuzuia washindani wa Vodacom.

Katika mkutano huo, watendaji wawili wa Kamati ya Ligi ambayo iko katika kipindi cha mpito kuelekea kuundwa kwa Bodi ya Ligi walitambulishwa kwa klabu hizo. Watendaji hao ni Silas Mwakibinga ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) na Joel Balisidya ambaye ni Ofisa wa Ligi (LO).

No comments:

Post a Comment