Thursday, September 20, 2012

FLAVIANA MATATA ANG'ARA WIKI YA MITINDO LONDON

Mwanamitindo wa kimataifa wa Tanzania, Flaviana Matata akiwa mzigoni katika pozi mbalimbali wakati wa maonyesha ya mavazi ya London
 

MWANAMITINDO maarufu nchini, Flaviana Matata ameendelea kupaa katika fani hiyo baada ya kung’ara katika maonyesho ya wiki ya Mavazi ya London, London Fashion Week.

Flaviana ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani kwa shughuli hizo za maonyesho mavazi, aliwavutia sana wadau wa maonyesho hayo akiwamo mwanamuziki nyota wa kike duniani, Stefani Joanne Angelina Germanotta maarufu kwa jina la Lady Gaga.

Mwanamitindo huyo aliwasisimua wadau wengi wa mitindo wakiwamo watu maarufu duniani na kuendelea kujizolea sifa na kutangaza jina lake na nchi yake pia.

Flaviana amekuwa akishiriki katika maonyesho hayo tangu mwaka 2010 na mwaka huu ameonyesha kukomaa zaidi.

Maonyesho ya mavazi ya mwaka huu yaliwahusisha wabunifu wengi maarufu wa mitindo ambapo mmoja wapo ni Vivenne Westwood  Red Label ambaye anatamba duniani.

Mbunifu Philip Treacy naye alifanya mambo makubwa katika maonyesho hayo yaliyozinduliwa na Lady Gaga.

Flaviana alipewa heshima kubwa ya kuvaa jaketi la mwanamuziki aliyekuwa mfalme wa muziki wa pop, marehemu Michael Jackson. Pia alivaa mavazi ya wabunifu maarufu kama Mike Fast na Christopher Raeburn.

Kutokana na jinsi alivyotamba katika maonyesho hayo, Flaviana alifanyiwa mahojiano na gazeti maarufu duniani la Marekani, Wall Street Journal.

Flaviana ambaye ni Miss Universe Tanzania wa mwaka 2007, aliipromoti nchi yake katika maonyesho hayo kama alivyofanya katika mashindano ya Miss Universe ya mwaka 2007 kwa kushika nafasi ya sita kati ya warembo 10 walioingia fainali. Mkurugenzi wa kampuni ya Compass Communications, Maria Sarungi Tsehai alisema kuwa anajisikia faraja kubwa kuona Flaviana anaendelea kufanya vyema katika fani hiyo.

No comments:

Post a Comment