Thursday, September 27, 2012

FAINALI ZA STR8 MUZIKI ZAFANA MWANZA


Izzo Bizness akishusha michano
 


FAINALI za tamasha la muziki la STR8 zilimalizika jana mjini hapa kwa kishindo cha aina yake huku tuzo ya DJ Bora yenye thamani ya thamani ya Sh. milioni 7 ikimuangukia DJ Juma Ramadhani.

Ilikuwa ni patashika nguo kuchanika wakati ma-DJ na ma-MC walipokuwa wakipambana vikali kuwania moja ya vifaa vya kisasa kabisa katika masuala ya kuchezesha muziki, DJ Pioneer.


Ruyobya Johaness a.k.a DJ YT alikamata nafasi ya pili katika kategori ya ma-MC akiondoka zawadi kadhaa zikiwamo fedha taslimu Sh.100,000.


Mshindi katika kategori ya MC alikuwa ni Joash Magadula ambaye pamoja na tuzo pia alipata nafasi ya kurekodi albamu katika moja ya studio tatu bora za muziki nchini.


Nchana Anthony alishika nafasi ya pili katika kategori hiyo ya ma-MC na aliondoka na zawadi kadhaa na fedha taslimu Sh.100,000.


Fainali hizo ambazo ni za tatu tangu zianzishwe nchini zinaratibiwa na kampuni ya Sigara nchini (TCC) kwa lengo la kukuza vipaji miongoni mwa vijana na kutengeneza nafasi ya ajira.


Michuano hiyo ambayo ilihusisha ma-Mc 85 na ma-DJ 25 zilichuja washindani wake hadi 16 kwa MC na 10 kwa ma-DJ katika raundi ya kwanza kabla ya raundi ya pili kutoa washiriki wa fainali.


Ma-DJ hao walipewa maksi kwa kuangaliwa na majaji kuhusu uwezo wao wa kuchanganya muziki, uwezo wa kiufundi, wanavyomudu vifaa wanavyofanyia kazi na jinsi wanavyoburudisha.


Ma-DJ sita waliofika fainali walikuwa Bernard Fabian, DJ Yt, Robert Rowan, DJ Megastar, Tony Wyclif na Juma Ramadhani.


Kategori ya MC ilihusisha mshiriki kupewa mada ya kuielezea kwa mtindo wa kufokafoka kwa dakika tatu kiushairi kimpangilio.


Matukio hayo ya fainali yalinogeshwa na burudani mbalimbali zikiwamo zilizotolewa na wakali wa Bongofleva kama rapa Izzo Bizness ambaye ni maarufu kupitia wimbo wake wa 'Riz-One (Ongea na Mshua)’ .


Walikuwapo pia vijana wa kundi la kudansi la BFB la Mwanza, ambao walipagawisha mashabiki kwa staili zao mbalimbali za kucheza ikiwamo kwa sarakasi.


Aliyetingisha zaidi katika vionjo alikuwa ni mshindi mwaka 2010 katika kategori ya MC, DJ Simba, ambaye alionesha ubabe wake katika kucheza na biti kiasi cha kufanya ukumbi mzima kurindima kwa shangwe.


“Vipaji hivi vinatakiwa kulelewa na kuendelezwa,” alisema Deogratius Kamugisha, mwenyeji wa mashindano hayo ambaye pia ni Meneja wa TCC Mwanza.


Alisema kwamba michuano hiyo ilikuwa si tu burudani bali pia ilitoa mwanya wa mafanikio mengine kama ajira.


Alisema washindi wa michuano iliyopita kwa sasa wako katika ajira mbalimbali zikiwemo vilabu vya usiku na vituo vya radio.


"Hii ni namna ya kutengeneza ajira," alisema na kuongeza kwamba mashine ya kuchezea muziki kama aliyopewa Juma Ramadhani ni chanzo cha ajira kwani anaweza kuitumia yeye au kuikodisha kwa wengine anapokuwa hana kazi nayo.


Mchuano mingine miwili itafanyika mjini Dar es Salaam na Mbeya kukamilisha tamasha la mwaka huu.

No comments:

Post a Comment