Saturday, September 1, 2012

CHELSEA WADHALILISHWA FAINALI SUPER CUP, WALALA 4-1, FALCAO APIGA 'HAT-TRICK'

Falcao akishangilia kwa kuonyesha ishara ya vidole vitatu baada ya kukamilisha 'hat-trick' yake dhidi ya Chelsea katika ushindi wa 4-1.

CHELSEA walisambaratishwa kabisa katika mechi yao ya fainali ya Kombe la Super Cup la Ulaya wakati Radamel Falcao alipofunga magoli matatu na kuisaidia Atletico Madrid kushinda 4-1 mjini Monaco.

Falcao angeweza kufunga angalau magoli MATANO peke yake kwani shuti lake jingine moja liligonga besela na pia kichwa chake kugonga nguzo ya goli katika mechi ambayo Chelsea walipotea kabisa na wangeweza hata kufungwa 10.

Alifunga goli la kwanza katika dakika ya 6, akakunja mpira kama 'ndizi' uliompita juu kipa Petr Cech katika goli lake la pili na akakamilisha la tatu kwa kumalizia shambulizi la kustukiza na kuongoza 3-0 kufikia mapumziko.

Miranda alifunga la nne katika kipindi cha pili kabla ya beki Gary Cahill kuwapa Chelsea la kufutia machozi kutokana na "gombania goli" ya mpira wa kona.

Katika mechi hiyo inayowakutanisha mabingwa wa Ulaya, Chelsea dhidi ya mabingwa wa Ligi ya Europa, walikuwa Atletico waliopata ushindi uliostahili huku Falcao akicheza katika kiwango kisichozuilika.

Straika huyo wa Colombia, ambaye alifunga magoli 24 katika Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) na magoli 12 katika michuano ya Ulaya msimu uliopita, aliingia katika mechi hiyo akitokea kupiga "hat-trick" nyingine katika mechi ya La Liga dhidi ya Athletic Bilbao waliyoshinda 4-0 na alitumia udhaifu wa beki inayokatika ya Chelsea.

Kufuatia kipigo kinachowadhalilisha vinara wa Ligi Kuu ya England, kocha wa Chelsea, Roberto Di Matteo alisema:

"Tulianza taratibu mno na tukaruhusu magoli mawili ndani ya dakika 20.

"Tuliacha wazi eneo kubwa (bila ya shaka akimaanisha hawakupaki basi). Hatukucheza kama staili yetu, ya kuwa wagumu kufungika, lakini leo jambo hilo halikuwepo.

"Hatukuwepo mchezoni kabisa, hivyo hilo ni jambo linalofadhaisha.

"Tuliwaachia nafasi kubwa mno Atletico Madrid, hasa mchezaji kama Falcao. Huwezi kumuachia nafasi."

Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone, alisema:

"Anachofanya Radamel ni baab'kubwa.

"Yeye ni mtu ambaye, ukimwekea malengo ya juu, anaenda juu zaidi.

"Nimemfahamu tangu akiwa kijana mdogo na daima ana njaa.

"Natumai, tunaweza kufurahia mambo yake Atletico kwa muda mrefu."

No comments:

Post a Comment