Friday, August 17, 2012

THOMAS VERMAELEN ATANGAZWA LEO NA KOCHA ARSENE WENGER KUWA NAHODHA MPYA WA KLABU YA ARSENAL

Vermaelen alishaanza kujifua mapema kuvaa 'tambara' la unahodha wa Arsenal... hapa akiwaongoza wenzake kuingia uwanjani kucheza dhidi ya Man City katika mechi yao ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya iliyochezwa jijini Beijing, China Julai 27, 2012.  

Unatisha kwa mabao kama mimi vile...! Aliyekuwa nahodha wa Arsenal, Robin van Persie akimpongeza Vermaelen kwa kumbeba baada ya beki huyo kutupia goli katika mechi yao mojawapo ya ligi kuu ya England msimu uliopita dhidi ya West Brom.Vermaelen amechaguliwa leo kutwaa mikoba ya Van Persie  

Kama straika vile...! Hapa Vermaelen akimtoka Zabaleta wa Man City wakati wa mechi yao ya kirafiki kujiandaa na msimu mpya iliyochezwa kwenye Uwanja wa Birds Nest Stadium jijini Beijing, China Julai 27, 2012.

Weeee...! licheki jembe Vermaelen linavyotuliza mpira. Bila shaka atakuwa nahodha wa ukweli!

Vermaelen akiondoka na mpira wakati wa mechi yao ya kirafiki kujiaandaa na msimu mpya dhidi ya Manchester City kwenye Uwanja wa Birds Nest Stadium jijini Beijing, China Julai 27, 2012.
LONDON, England
Thomas Vermaelen amechaguliwa kurithi mikoba ya Robin van Persie kwa kuwa nahodha wa Arsenal kuanzia leo, kocha Arsene Wenger amesema.

Baada ya kuondoka kwa Van Persie aliyehamia Manchester United, kocha huyo Mfaransa alikuwa makini kutangaza mapema jina la nahodha mpya kabla ya mechi yao ya kesho Jumamosi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Sunderland.

Mikel Arteta ametajwa na Wenger kuwa nahodha msaidizi katika msimu wake wa pili tu klabuni hapo baada ya kusajiliwa katika dirisha lililopita la usajili wa majira ya kiangazi akitokea Everton.

"Nahodha mpya ni Vermaelen na (nahodha msaidizi ni) Arteta," Wenger amewaambia waandishi wa habari.

"Tuna wachezaji wengi wenye sifa za kutwaa unahodha katika timu hii."

Vermaelen alijiunga na Arsenal akitokea Ajax ya Uholanzi Juni, 2009, na kiwango chake cha juu kimempa umaarufu mkubwa miongoni mwa mashabiki wa klabu hiyo, akifunga goli katika mechi yake ya kwanza akiwa Arsenal waklati walipocheza dhidi ya Everton na kisha akafunga magoli mengine kadhaa katika msimu wake huo wa kwanza.

Baada ya kuwa nje kwa vipindi kadhaa kutokana na majeraha, beki huyo wa kimataifa wa Ubelgiji alirejea uwanjani kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita na kuwa na ushirikiano mzuri na Laurent Koscielny katika kulinda lango la timu yao.

Arsenal watawakaribisha Sunderland kesho mchana (saa 11:00 jioni kwa saa za Tanzania) kwenye Uwanja wa Emirates wakati ikiwa na matumaini ya kumaliza katika nafasi nzuri zaidi ya msimu uliopita ambapo walikamata nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, na Wenger anajua kwamba wanakabiliwa na kibarua kigumu katika mechi yao ya ufunguzi.

Amesema: "Kwa kawaida, mechi dhidi yao (Sunderland) siku zote huwa ngumu, na tena ya kutumia maguvu. Sisi tunachopaswa kufanya ni kujitengenezea nafasi."

No comments:

Post a Comment