Wednesday, August 1, 2012

SOMA TAARIFA YA MNYIKA KUHUSU RUFAA YAKE KATIKA TUHUMA ZA EPA DHIDI YA MWIGULU NCHEMBA NA JINSI ALIVYOMCHANA MWENYEKITI JENISTA MHAGAMA


RUFAA YANGU KATIKA TUHUMA ZA EPA NA MWIGULU NCHEMBA 

Mhe. John Mnyika
Mhe. Mwigulu Nchemba
Mhe. Jenista Mhagama
Na John Mnyika
Nimekata Rufaa dhidi ya uamuzi wa Mwenyekiti Mhagama suala la EPA; nasubiria Spika aitishe kamati ya kanuni ili bunge liendeshwe kwa ufanisi:
Katika kipindi cha takribani wiki mbili nimeulizwa kwa nyakati mbalimbali na wananchi kwenye mitandao ya kijamii na wanahabari kwa njia ya simu kutaka kufahamu iwapo nilitimiza azma ya kukata rufaa juu ya uamuzi wa Mwenyekiti wa Bunge Jenister Mhagama kutoa muongozo wa kunitaka kuwasilisha ushahidi katika suala alilolisema yeye mwenyewe badala ya kunipa fursa ya kueleza tuhuma nilizonazo dhidi ya Mwigulu Nchemba na hatimaye kuwasilisha ushahidi juu ya tuhuma hizo.
Kwa kuwa swali na suala hilo limekuwa likirudiwarudiwa kwenye mijadala mbalimbali bila taarifa sahihi kutolewa, naomba kutoa majibu kwamba tayari nilishawasilisha malalamiko kwa mujibu wa Kanuni ya 5(4) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toka tarehe 12 Julai 2012 dhidi ya uamuzi huo wa Mwenyekiti wa Bunge ambao haukuzingatia matakwa ya Kanuni za kudumu na uendeshaji bora wa Bunge.
Ninachosubiria sasa ni Spika kuitisha kikao cha kamati ya kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5(5) ya kanuni za Kudumu za Bunge na kulijulisha bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa.
Nimekata rufaa kwa sababu tatu:  mosi; mwenyekiti amenitaka kuwasilisha ushahidi wa suala ambalo sikulisema mimi bali amelisema yeye; pili, Sikupewa nafasi ya kueleza tuhuma nilizotaka kueleza dhidi ya Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba na badala yake Mwenyekiti aliendelea kunitaka nizungumzie tuhuma alizozieleza yeye; mwenyekiti hakufanya uamuzi kuhusu suala ambalo nililiombea kuhusu utaratibu kwa mujibu wa kanuni ya 64 (1) (a) juu ya madai ya Mwigulu Lameck Nchemba juu ya hotuba ya kambi rasmi ya upinzani ya Ofisi ya Rais.
Katika barua yangu kwa katibu wa Bunge nilieleza pia kuwa ni muhimu kamati ya kanuni ikakutana kabla ya kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kushughulikia uamuzi uliofanywa na Naibu Spika Job Ndugai tarehe 12 Julai 2012 katika kikao cha ishirini na mbili cha mkutano wa nane kwamba “Kamati hiyo sasa ndiyo itashughulikia ushahidi huo na kuthibitisha kwamba Mheshimiwa Mwigulu  naye kumbe alikuwa anahusika na wizi wa fedha za EPA”, ili kamati hiyo isifanye uamuzi kwa kurejea muongozo usiokuwa sahihi.
Ikumbukwe kwamba kwa mujibu wa  kumbukumbu rasmi ya Bunge (Hansard) za kikao cha kumi na tano cha tarehe 3 Julai 2012 cha mkutano wa nane wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwenyekiti wa Bunge Jenister Mhagama alisema na kufanya maamuzi kwamba: “Mheshimiwa Mnyika, umesema kwamba unao ushahidi, naomba unisikilize kusudi utakaponijibu ujibu mwongozo nitakaokupa kwa mujibu wa taratibu. Mheshimiwa Mnyika umesema hapa na kulithibitishia Bunge, waheshimiwa wabunge naomba tusikilizane. Umesema unao ushahidi na umelithibitishia Bunge kwamba yeye Mheshimiwa Lameck Mwigulu Nchemba ni mmoja wa watuhumiwa katika kesi hizo za EPA. Sasa na mimi nakupa siku saba ulete ndani ya Bunge tuhuma zinazomgusa Mheshimiwa Mwigulu.”
Katika rufaa yangu nimeeleza kutoridhika dhidi ya  muongozo huo wa Mwenyekiti wa Bunge na kwa kutumia kanuni ya 5 (4) nimewasilisha sababu za kutoridhika na uamuzi huo kama ifuatavyo:
Sababu ya Kwanza; Mwenyekiti amenitaka kuwasilisha ushahidi wa suala ambalo sikulisema mimi bali amelisema yeye:
Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge sikutamka maneno kwamba ninao ushahidi wa kulithibitishia bunge kwamba Lameck Mwigulu Nchemba ni mmoja wa watuhumiwa wa kesi hizo za EPA  kama ambavyo amedai Mwenyekiti wa Bunge kama nilivyomnukuu hapo juu.
Nilichokisema, na nanukuu: 
“Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nasimama kwa kanuni ya 64 (1) (a) hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli, Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji anayezungumza ili aelewe kwamba anachokisema anakitambua; alikuwa mtumishi wa Benki Kuu ambayo ilikumbwa na kashfa ya ufisadi wa EPA na sasa ni Mweka Hazina wa Chama cha CCM inayotuhumiwa kwenye wizi wa pesa za KAGODA... lakini usalama wa taifa hatujawahi kusikia popote katika kuzuia. Usalama wa Taifa kuhusika kwenye kuzuia. Kwenye Bunge hili, kambi ya upinzani ilileta ushahidi wa Barua ya usalama wa Taifa kwenye kashfa hiyo ya EPA ambayo anaifahamu vizuri . Usalama wa taifa ukizuia jambo lisije bungeni kujadiliwa badala ya kuibua ufisadi, kuzuia ufisadi usitokee, ushahidi huo uko ndani ya kumbukumbu za Bunge na ukitaka nilete ushahidi wa namna gani matukio ya uhalifu na hili ni lalamiko ndani ya idara ya usalama wa taifa ya watumishi wa usalama wa taifa wanatoa ushirikiano ,wanatoa taarifa viongozi wa juu yao hawazishughulikii  taarifa  na katika hotuba ya ofisi ya rais haijatuonyesha popote idara ya usalama wa taifa ilipozuia matukio ya uhalifu kwenye hotuba hii tunayozungumza. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba mchangiaji atambue huo ukweli na aache propaganda na aache siasa kwa sababu yeye ni mmoja wa watuhumiwa”
Sababu ya Pili; Sikupewa nafasi ya kueleza tuhuma nilizotaka kueleza dhidi ya Mwigulu Lameck Nchemba na badala yake Mwenyekiti aliendelea kunitaka nizungumzie tuhuma alizozieleza yeye.
Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) niliposema “aache propaganda  na aache siasa kwa sababu yeye ni mmoja wa watuhumiwa”, Mwenyekiti aliingilia kati kabla ya mimi kueleza kuwa yeye ni mmoja wa watuhumiwa wa nini na kuelekeza ifuatavyo:
 “Mheshimiwa Mnyika, naomba uthibitishe hilo kwamba na yeye ni mmoja wa watuhumiwa kabla sijatoa mwongozo na kama unao uthibitisho kwamba na yeye ni mmoja wa watuhumiwa naomba utoe uthibitisho huo kama huna ufute kauli yako ili niweze kufanya maamuzi ya kinachofuata ili tuendelee na kazi za kuwawakilisha wananchi. Mheshimiwa Mnyika una uthibitisho wa kwamba Mheshimiwa Mwigulu ni mmoja kati ya wanaotuhumiwa?
Nilipoanza tu kueleza kuwa:“Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuwa mmoja wa watumishi wa Benki Kuu...” kabla hata ya kuendelea kueleza ni mtuhumiwa wa nini katika taasisi ambazo nilitaka yeye alizitumikia au anaendelea kuzitumikia Mwenyekiti akanikatisha na kudai yafuatayo “Mheshimiwa Mnyika umesema hapa na kulithibitishia (bunge)”.
Ilibidi niingilie kati na kuomba tena haki ya kueleza ni Mwigulu Lameck Nchemba ni mmoja kati ya wanaotuhumiwa na nini kwa kumuomba Mwenyekiti anipe haki ya kujieleza na kueleza tuhuma kama ifuatavyo:
“Niambie kwanza niseme tuhuma gani ninazo dhidi yake na nitoe ushahidi wa hizo tuhuma. Nimesema ni mmoja wa watuhumiwa. Niruhusiwe niseme anazotuhuma gani na nitoe ushahidi wa hizo tuhuma.”
Hata hivyo Mwenyekiti alikataa kunipa nafasi ya kueleza tuhuma nilizotaka kueleza dhidi ya Mwigulu Lameck Nchemba na badala yake Mwenyekiti akafanya uamuzi wa kunitaka nilete ushahidi wa tuhuma alizozieleza yeye.
Sababu ya Tatu; Mwenyekiti hakufanya uamuzi kuhusu suala ambalo nililiombea kuhusu utaratibu kwa mujibu wa kanuni ya 64 (1) (a) juu ya madai ya Mwigulu Lameck Nchemba juu ya hotuba ya kambi rasmi ya upinzani ya Ofisi ya Rais:
Nilitaka utaratibu ili aweze kuondoa maneno potofu aliyoyatoa huu ya nukuu juu ya ukweli ambao kambi rasmi ya upinzani iliueleza kwamba “…. Usalama wa Taifa hatujawahi kusikia popote wamehusika katika kuzuia mchakato huo japokuwa wanakuwa na taarifa za kutosha.”
Hata hivyo, Mwenyekiti hakufanya uamuzi kuhusu suala hilo ambalo nilitangulia mimi kuliomba badala yake akaishia kunitaka kuleta ushahidi wa tuhuma alizozieleza yeye mwenyewe mwenyekiti bila kufanyia kazi utaratibu ambao niliomba uzingatiwe. Hali ambayo inaweza kutafsiriwa kuwa ulikuwa ni upendeleo kwa Mwenyekiti hakumkatisha Nchemba alipotoa tuhuma dhidi ya kambi rasmi ya upinzani kumtaka athibitishe alipotajwa tu ni mmoja wa watuhumiwa bila tuhuma hizo kuelezwa Mwenyekiti alitoa muongozo wa tuhuma alizozisikia yeye na kutaka ushahidi uletwe kwa tuhuma hizo.
Pamoja na kuwawakilisha wananchi katika masuala mengine ya maendeleo bungeni, hatua hii ya kukata rufaa inalenga kudumisha ukweli na kuhakikisha kwamba bunge linaendeshwa kwa kuzingatia kanuni bila upendeleo ili kuweza kutimiza wajibu wa kikatiba wa kuisimamia serikali kwa ufanisi zaidi.
Wako katika kuwawakilisha wananchi,

John Mnyika (Mb)

No comments:

Post a Comment