Friday, August 24, 2012

SOMA KILA KITU KUHUSU MECHI ZA LIGI KUU YA ENGLAND WIKIENDI HII... EVRA KUCHEZA BEKI WA KATI, LIVERPOOL WANAMALIZANA NA SAHIN, WENGER ASEMA ATASAJILI...

Nuri Sahin... Jembe linalotua Liverpool

LONDON, England
HABARI kuhusu mechi za Ligi Kuu ya England wikiendi hii:

Liverpool wamesema kwamba wanatarajia kukamilisha uhamisho wa kiungo wa Real Madrid, Nuri Sahin kwa mkopo kabla ya mechi yao ya Jumapili dhidi ya mabingwa Manchester City (itakayoanza saa 1:00 usiku)

"Tunatumai ndani ya saa 24 tutakuwa tumeshapata uthibitisho katika suala hilo," kocha Brendan Rodgers alisema jana baada ya kuhusu ushindi wa Kombe la Europa dhidi ya Hearts ya Scotland.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uturuki alikuwa nguzo muhimu katika kuisaidia Borussia Dortmund kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani ya Bundesliga katika msimu wa 2010/11 lakini amecheza mara chache sana akiwa na Real msimu uliopita.

Evra huenda akacheza beki wa kati

EVRA KUCHEZA BEKI WA KATI

Manchester United, ambao wanakabiliana na Fulham Jumamosi (saa 12:00 jioni), wana tatizo na majeruhi katika safu yao ya ulinzi huku Jonny Evans, Rio Ferdinand na Chris Smalling wote wakiwa bado nje ya uwanja na Phil Jones hajawa fiti bado kwa ajili ya mechi.

Kocha Alex Ferguson amesema anafikiria kumchezesha Patrice Evra kama beki wa kati, huku mchezaji mpya waliyemsajili Alexander Buttner akitarajiwa kuanzia benchi.

"Evra huenda akacheza kama beki wa kati. Ameshawahi kufanya hivyo siku za nyuma," Ferguson aliwaambia wanahabari.

Adebayor amebeba matumaini ya AVB baada ya Spurs kuanza na kipigo cha 2-1.

AVB AMTARAJIA ADEBAYOR AMBEBE
Kocha wa Tottenham Hotspur, Andre Villas-Boas amesema anamtarajia Emmanuel Adebayor awe na mchango mkubwa baada ya uhamisho wake wa kutokea Manchester City kukamilika kuelekea mechi yao ya Jumamosi dhidi ya West Bromwich Albion (itakayochezwa saa 12:00 jioni).

"Alikuwa na msimu mzuri sana hapa msimu uliopita na ni kama tayari ni mmoja wa familia yetu. Kile atakachofanya kwa ajili yetu kinafahamika wazi," alisema Villas-Boas.

Straika huyo wa Togo aliichezea Tottenham kwa mkopo msimu uliopita.

Beki Younes Kaboul atakosa kutokana na majeraha ya goti wakati Spurs ikisaka ushindi wake wa kwanza msimu huu baada ya kipigo cha 2-1 ugenini dhidi ya Newcastle United wiki iliyopita.

Demba Ba... hatihati kuivaa Chelsea. Nadhani wanaombea iwe hivyo maana huyu "mdudu" "hafwai"....

DEMBA BA KUWAKOSA CHELSEA?
Newcastle watafanya maamuzi ya dakika za lalasalama kama wamjumuishe nahodha Fabricio Coloccini na straika Demba Ba kwa ajili ya mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Stamford Bridge (itakayoanza saa 2:30 usiku).

Wawili hao walikosa mechi ya Alhamisi ya Ligi ya Europa dhidi ya Atromitos kutokana na majeraha ya paja na ugoko. Cheick Tiote (kiazi cha mguu) na Shola Ameobi (misuli ya nyuma ya paja) pia wako shakani.

Nahodha wa Chelsea, John Terry yuko shakani kucheza baada ya kuumia shingo dhidi ya Reading Jumatano, kocha Roberto Di Matteo alisema.

Beki Cesar Azpilicueta amekuwa mchezaji wa tano kusajiliwa chini ya Di Matteo katika kipindi hiki cha usajili wakati alipojiunga jana akitokea Olympique Marseille, huku Victor Moses akijiandaa kufanyiwa vipimo vya afya baada ya kuafikiana ada ya uhamisho na Wigan Athletic.


Chamberlain... amerejea mazoezini huenda akacheza

WENGER AWEZA KUSAJILI

Kocha Arsene Wenger amesema kuelekea mechi ya Arsenal ugenini dhidi ya Stoke Jumapili (itakayoanza saa 10:30 jioni) atafikiria kuongeza wachezaji wapya kabla ya dirisha halijafungwa Ijumaa ijayo, lakini iwapo tu kama kutakuwa "kitu spesho sokoni".

"Staili yangu ni kwamba tuna kikosi ngangari sana lakini kama kutakuwa na fursa moja ama mbili tutaichangamkia," aliwaambia wanahabari.

Alex Oxlade-Chamberlain ana nafasi ya kucheza baada ya kurejea mazoezini, wakati kipa Wojciech Szczesny aliye na shaka kidogo ya majeraha anaweza kucheza. Laurent Koscielny bado yuko nje kutokana na majeraha ya kiazi cha mguu.

No comments:

Post a Comment