Sunday, August 5, 2012

SIMBA YAANZA NA SARE LIGI SUPER 8

SIMBA ya Dar es Salaam iliyochezesha kikosi B imetoka sare ya 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Pemba katika mechi yao ya ufunguzi ya Ligi ya Super 8 kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam leo jioni.

Katika mechi ambayo Simba ilitawala na kupoteza nafasi nyingi za kufunga, Jamhuri ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Bakari Khamis aliyeifungia timu yake katika dakika ya 48 kufuatia krosi ya Abdallah Othman.

Wakati mechi ikionekana kulala kwa matokeo ya 1-0, nahodha wa Simba wa leo, Shomary Kapombe, ambaye alikuwa mchezaji pekee wa timu A, aliisawazishia timu yake kwa njia ya penalti katika dakika ya 83 iliyotokana na Miraj Adam kuangushwa kwenye eneo la hatari na Mfaume Shabani wa Jamhuri.

Michuano hiyo  iliyogawa katika makundi mawili inashirikisha timu nane, ambapo Kundi A lina timu za Simba, Jamhuri, Zimamoto na Mtende FC, wakati Kundi B lina timu za Super Falcon, Azam FC, Mtibwa Sugar na  Polisi Moro.

Bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Bank ABC ataondoka na zawadi ya Sh. milioni 40, mshindi wa pili Sh. milioni 20, wa tatu Sh. milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. milioni 5 kila moja.

Michuano itachezwa katika vituo vinne vya Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na Mwanza, ambapo timu zitasafirishwa kwa ndege kwenda kucheza mechi katika vituo vyote. Kila timu itacheza mechi mechi katika vituo vituo vitatu tofauti. Simba baada ya mechi ya leo, itakwea pipa kwenda Arusha kucheza dhidi ya Mtende FC Alhamisi na itasafiri kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi yao ya mwisho ya Kundi A dhidi ya Zimamoto Jumamosi.


No comments:

Post a Comment