Sunday, August 5, 2012

SAMATTA APIGA LA 4 KLABU BINGWA AFRIKA, MGHANA CLOTTEY KINARA WA MABAO, ABOUTRIKA, MPUTU No.2


Straika Samatta akifanya vitu vyake jana kabla kutupia goli 'kali' la kichwa.

Straika Samatta akiokota mpira wavuni baada ya kuifungia Mazembe katika mechi mojawapo ya Klabu Bingwa Afrika.
LUBUMBASHI, Kongo
Mbwana Samatta amepanda hadi katika nafasi ya tatu ya wakali wanaoongoza kwa kupachika mabao katika Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kupiga goli kali la kichwa na kuisaidia klabu yake ya TP Mazembe ya Kongo kuibuka na ushindi ‘mtamu’ wa mabao 2-0 dhidi ya Zamalek ya Misri katika mechi yao ya Kundi B iliyochezwa jana mjini Lubumbashi.

Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa hazijafungana. Kiungo Ngandu Kasongo aliifungia Mazembe bao la utangulizi katika dakika ya 70.

Wenyeji walipata bao la pili dakika saba baadaye wakati straika wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samata alipowazidi ujanja mabeki wa Zamalek kwa kuruka juu peke yake kuuwahi mpira wa 'fri-kiki' kutoka kushoto mwa uwanja na kufunga bao safi la kichwa lililokuwa la nne kwake katika michuano hiyo msimu huu.

Maelfu ya mashabiki waliojazana kwenye uwanja mpya wa Mazembe mjini Lubumbashi unaoingiza watu 15,000 walilipuka kwa shangwe kutokana na bao la Samatta lililowapa matumaini ya kupata pointi zote tatu.


Ushindi huo uliipaisha Mazembe hadi katika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi lao la B kufuatia wapinzani wao katika kuwania nafasi hiyo, klabu ya Berekum Chelsea ya Ghana, kukubali kipigo kizito cha ugenini cha mabao 4-1 kutoka kwa vinara Al Ahly.

Katika msimamo, Al Ahly wanaongoza wakiwa na pointi tisa baada ya kushinda katika mechi zote tatu na kufuatiwa na Mazembe wenye pointi nne, sawa na Chelsea lakini Waghana wakizidiwa na akina Samatta kwa tofauti ya mabao.

Kipigo kutoka kwa Mazembe kilizidi kuichimbia mkiani klabu ya Zamalek isiyokuwa na pointi baada ya kufungwa katika mechi zote, na ambayo kabla ya mechi hiyo iliachana na kocha Hassan Shehata aliyeamua kubwaga manyanga kutokana na mfululizo wa matokeo mabaya.

Ushindi pia umeongeza matumaini ya Mazembe kutinga nusu fainali kwani timu mbili za kundi lao la B na nyingine za idadi hiyo kutoka Kundi A ndizo zitakazosonga mbele kwa hatua inayofuata.


Baada ya bao lake la nne jana, Samatta amepanda katika orodha ya majina ya wanaoongoza kwa ufungaji na kushika nafasi ya tatu, akitanguliwa na Mghana Emmanuel Clottey wa Berekum Chelsea aliyeongeza bao jingine jana wakati timu yake ikilala 4-1 na hivyo kufikisha mabao 12 huku Mohamed Aboutrika wa Ahly na Tressor Mputu (TP Mazembe) wakikamata nafasi ya pili baada ya kila mmoja kufikisha magoli sita.

Clottey amebakiza bao moja kufikia rekodi ya mabao katika historia ya michuano hiyo iliyowekwa msimu wa 2007 na Mnigeria Stephen Worghu.

Orodha ya wakali wa mabao katika Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya mechi za jana:

12 Emmanuel Clottey    (Berekum Chelsea)
  6 Tresor Mputu           (TP Mazembe)
     Mohamed Aboutrika (Al-Ahly)
  4 Mbwana Samatta     (TP Mazembe)  
     Karim Ali Hadji         (ASO Chlef)
     Rasca                      (Recreativo do Libolo)
     Izu Azuka                (Sunshine Stars)
     Mudather El Tahir   (Al-Hilal )
    Youssef Msakni               (EspĂ©rance)
 3 Mohamed Seguer    (ASO Chlef)
   Jacques Haman       (Coton Sport)
   Oumar Kida             (Stade Malien)
   Muandro                  (Muculmana)
   Stelio Telinho           (Muculmana)
   Ifeanyi Egwim          (Dolphins)
   Edward Sadomba    (Al-Hilal)
   Kelechi Osunwa       (Al-Merreikh)
   Lasaad Jaziri            (Etoile du Sahel)
   Felix Nyaende          (Power Dynamos)
   Takesure Chinyama (Dynamos-Zimbabwe)


CAIRO, Matokeo na msimamo wa Kundi B la Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya mechi za jana Jumamosi, Agosti 4  

Al Ahly Cairo (Misri)            4  Berekum Chelsea (Ghana)  1
TP Mazembe (DR Congo)   2  Zamalek (Misri)                   0
 
                                   P W D L  F  A Pts
1 Al Ahly Cairo            3  3  0  0  7  2  9 
2 Berekum Chelsea    3  1  1  1  6  8  4 
3 TP Mazembe            3  1  1  1  5  4  4 
4 Zamalek                   3  0  0  3  2  6  0


No comments:

Post a Comment