Friday, August 10, 2012

REHMTULLAH KUZINDUA MITINDO MIPYA

Mbunifu wa mitindo ya mavazi, Ally Rehmtullah akionyesha moja ya mavazi aliyobuni.
Mbunifu wa mitindo ya mavazi, Ally Rehmtullah akionyesha moja ya mavazi aliyobuni.
Mbunifu wa mitindo ya mavazi, Ally Rehmtullah akionyesha moja ya mavazi aliyobuni.
Bango la onyesho la mitindo ya mavazi la Ally Rehmtullah linavyoonekana.

Na Mwandishi Wetu
MWANAMITINDO maarufu nchini Ally Rehmtullah ameandaa onyesho kubwa na la kipekee la mitindo  litakalofanyika Septemba 8 jijini Dar es Salaam, ambalo litarushwa moja kwa moja katika mtandao wa www.ar.co.tz bure.

Akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari hivi, Rehmtullah alisema dhumuni la kuandaa onyesho hilo la kipekee ni kuonyesha aina mpya ya mitindo ya mavazi aliyobuni hivi karibuni na harakati zake za kuinua kiwango cha kazi za mitindo ndani ya nchi.

“Nimepania kupanua wigo wa taaluma ya mitindo na mavazi hapa nchini ili kazi za wanamtindo na wabunifu wa mavazi nchini ziweze kupenya kwenye soko la ndani na la Afrika Mashariki na Kati wakati tayari kuna soko la pamoja katika jumuiya ya Afrika mashariki," alisema.

Rehmtullah alisema kwamba onyesho hilo litakuwa la kipekee kwa sababu mavazi na onyesho litapambwa na rangi nyeupe, ubunifu wa hali ya juu pamoja na muonekano mpya wa mavazi yaliyofanyiwa utafiti mkubwa ili kuendana na utamaduni wa mwafrika.

Alisema onyesho hilo ambalo litafanyika katika hoteli ya Serena litapambwa na wasanii mbalimbali wa muziki na wacheza shoo toka sehemu mbalimbali hapa nchini.

Rehmtullah alisema onyesho hilo itakuwa ni nafasi ya kipekee kwa yeye binafsi kuonyesha muonekano mpya wa tasnia ya mitindo nchini na nje ya nchini ili kuonyesha ni kwa jinsi gani wanamitindo wa Kitanzania wanavyoimudu fani ya mitindo.

Alisema kuwa tasnia ya mitindo kwa ujumla ina nafasi ya kipekee kwa wanamtindo chipukizi nchini kujitokeza na kuonyesha kazi zao kwa watu mbalimbali hasa wadau katika sekta hiyo.

"Kazi za mitindo na mavazi ndio mkombozi wa kweli katika kupunguza tatizo la ajira nchini Tanzania kwa sababu ni sekta inayokua kwa kasi kubwa na inatoa ajira kwa vijana wengi wa kike na kiume," aliongeza.

Onyesho hilo linategemewa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 400 wakiwemo viongozi mbalimbali kama mawaziri, wabunge, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mashirika mbalimbali.

Onyesho hilo litakuwa ni la mialiko maalum na limepewa jina la Ally Rehmtullah 2013 Collection.

Wadhamini wa onyesho hilo ni Mercedez Benz, Belvedere Vodka, DULUX, RAHA, HUGO DOMINGO,THE Tanzanite Experience, Shiva Images, Farm Plant, Creative Infinities, Out Door, Stanbic Bank, Phoenicia Properties, Dar es Salaam Serena Hotel, Missie Popular Blog, Mo Blog, Quality Furniture na Mx Carter.

No comments:

Post a Comment