Friday, August 3, 2012

REAL MADRID SASA KUMTWAA LUIS NANI KWA BIL. 46/-


Luis Nani
MADRID, Hispania
Mwanzo ilionekana kama utani. Lakini sasa imebainika kuwa kweli Real Madrid wamepania kutekeleza mkakati wao wa kurundika nyota kikosini kwa sera ileile ya ileile ya ‘Ki-galactico’ baada ya kujulikana mchana huu kwamba wako tayari kutuma ofa nono ya kumtwaa winga Luis Nani wa klabu ya Manchester United.

Hata hivyo, vyanzo kutoka Urusi vimesema kuwa Real Madrid ya kocha Jose Mourinho bado iko katika mapambano makali ya kumtwaa winga huyo wa kimataifa wa Ureno kwavile matajiri wa klabu ya Anzhi pia wamepania Nani, ambaye bado hajakubali kusaini ofa ya mkataba mpya alioongezewa na Man U licha ya kuwahi kufanya nao mazungumzo ya kina mwanzoni mwa mwaka huu.

Taarifa za mchana huu zinadai kwamba sasa Real wako tayari kutuma ofa ya awali ya paundi za England milioni 19 ili kuiulainisha Man U na kumtwaa Nani ambaye ushirikiano wake na Cristiano Ronaldo unatarajiwa kuongeza makali ya mabingwa hao wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania, kama walivyoonyesha wakati wa fainali za Euro 2012 ambapo waliifikisha nusu fainali timu yao ya taifa ya Ureno na kukosa fainali ‘kiduchu’ baada ya kutolewa kwa matuta na waliokuja kuwa mabingwa, timu ya taifa ya Hispania.

Mbali na kuwa tayari kwa kumwaga ‘mkwanja’, imeelezwa kuwa faida ya ziada waliyo nayo Real Madrid katika vita ya kumuwania Nani ni ukweli kwamba wakala anayemsimamia kocha wao Jose Mourinho na wachezaji wao nyota kama Ronaldo, Pepe, Fabio Coentrao na Marcelo, ndiye huyohuyo pia anayemuwakilisha Luis Nani!

No comments:

Post a Comment