Tuesday, August 28, 2012

REAL MADRID, BARCA UTATAMANI KESHO IFIKE.... NGOMA KUPIGWA SAA 5:30 USIKU, SONG, MODRIC HUENDA WAKACHEZA

Lionel Messi wa Barcelona (wa pili kulia) akilindwa na msitu wa wachezaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo (kushoto), Fabio Coentrao (wa pili kusho) na Xabi Alonso wakati wa mechi yao ya kwanza ya mechi ya Super Cup kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Agosti 23, 2012. Barca ilishinda 3-2.

KUZINDUKA kutoka katika kipigo na kutwaa taji la Super Cup la Hispania dhidi ya mahasimu wao Barcelona pamoja na kuwasili kwa kiungo mchezesha timu wa Croatia, Luka Modric huenda kukaleta mwanzo mzuri sana wa msimu kwa Real Madrid.

Kikosi kilichojaa nyota cha Jose Mourinho, bado kinasaka ushindi wa kwanza wa ligi msimu huu, kinahitaji kupiku kipigo cha 3-2 kutoka katika mechi yao ya kwanza wakati watakapowakaribisha Barca kwenye Uwanja wa Bernabeu kesho.

Kipigo cha kustusha cha 2-1 kutoka kwa majirani wa mji mmoja ugenini Getafe kilikuja baada ya sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Valencia katika mechi yao ya ufunguzi wa La Liga.

Mourinho aliyejawa na hasira hakuficha kitu wakati alipoongea katika mkutano na wanahabari baada ya mechi hiyo, akiita kiwango walichoonyesha dhidi ya Getafe kuwa ni "kibovu kabisa".

Real walistahili kufungwa na kiwango chao kilikuwa hakikubaliki, Mreno huyo alisema, akiongeza kwamba alikerwa na magoli mawili waliyoruhusu dhidi ya Valencia na Getafe kutokana na mipira ya adhabu ndogo.

"Tulijaribu kufanya kilicho bora lakini tunakubaliana na kocha kwamba hakikuwa kiwango kizuri," alisema  nahodha na kipa Iker Casillas.

"Ni mechi ambayo tunahitaji kuisahau na kuweka akili katika mechi ijayo. Hivi sasa ni Super Cup na tutakuwa na fursa ya kujirekebisha na kusahau mechi hizi zote tatu."

Real ilitangaza Jumatatu kwamba wameafiki kumsajili Modric kutoka Tottenham Hotspur kwa mkataba wa miaka mitano na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye ubunifu alionao ni kati ya mambo ambayo kikosi cha Mourinho kimekuwa kikiyakosa msimu huu.

Modric alionyesha kiwango cha juu kwa timu yake ya taifa ya Croatia dhidi ya Hispania katika mechi ya hatua ya makundi ya Euro 2012 ambayo walilala 1-0 na huenda akachuana tena na na nyota wa Hispania wanaochezea Barca, Xavi, Gerard Pique, Jordi Alba na Sergio Busquets kama atapangwa leo.

MESSI 'HAFAI-HAFAI'
Barca wanajiachia kileleni mwa msimamo wa La Liga baada ya kushinda mechi zao mbili za kwanza, ambazo kwa kiasi kikubwa shukrani ziende kwa "u-jinias' wa Mwanasoka Bora wa Mwaka, Lionel Messi.

Mshambuliaji huyo wa Argentina amefunga magoli matano katika mechi tatu za michuano yote ikiwamo penalti katika mechi ya kwanza ya Super Cup na magoli yote mawili katika ushindi wa Jumapili wa 2-1 ugenini Osasuna, ikiwa ni mwanzo bora zaidi wa msimu kwake.

Messi (25) amefunga magoli 31 katika mechi 17 zilizopita za Barca katika ligi kuanzia msimu uliopita na amebakisha magoli 17 tu kuifikia rekodi ya klabu hiyo ya kufunga magoli 190 ya ligi inayoshikiliwa na Cesar Rodriguez.

"Msimu unaweza kuwa hatujaanza vizuri sana... lakini timu iko vizuri," alisema Pique.

Kocha wa Barca, Tito Vilanova ana maswali kuhusu nahodha na beki wa kati Carles Puyol baada ya kuumia mfupa wa chini ya jicho katika mechi yao dhidi ya Osasuna.

Mchezaji mpya waliyemsajili Alex Song huenda akapewa mechi yake ya kwanza baada ya kiungo huyo wa Cameroon kujiunga akitokea Arsenal wiki iliyopita.

Real wanasubiri uzima wa beki wa Ureno, Pepe ambaye hajacheza tangu alipopata majeraha ya kichwa dhidi ya Valencia.

No comments:

Post a Comment