Tuesday, August 14, 2012
POULSEAN AMWAGA TAMBO ZA USHINDI BOTSWANA
Na Mwandishi Maalumu, Gaborone
KOCHA wa ya timu ya taifa ya soka ya Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kuwa amewaandaa wachezaji wake vizuri kisaikolojia kwa ajili ya kushinda mechi ya kesho dhidi ya The Zebras ya Botswana.
Stars, ambayo inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, iliwasili mjini Gaborone nchini Botswana leo saa 5:30 asubuhi kwa saa za Botswana na saa 6:30 mchana kwa saa za Afrika Mashariki na kupata mapokezi mazuri kutoka kwa viongozi wa serikali pamoja na Watanzania wanaoishi hapa.
Akizungumza na wanahabari jijini Gaborone leo, Kim alisema kwamba timu iko vizuri na kila mchezaji ana morali kubwa ya kushinda mechi hiyo.
"Nimezungumza na mchezaji mmoja mmoja nikazungumza na timu nzima na kuwaeleza juu ya umuhimu wa mechi hii,” alisema Kim.
"Baada ya kuzungumza nao wamenielewa na kutambua kuwa kukosekana kwa washambuliaji watatu katika timu hiyo ambao ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na John Bocco 'Adebayor', hakuwezi kuwafanya washindwe kucheza na kuibuka na ushindi."
Alisema kwamba anatambua kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu Botswana ni timu nzuri na inajiandaa kwa mashindano ya Afrika pamoja na mashindano ya Kombe la Dunia kama ilivyo kwa Stars hivyo kila timu inahitaji ushindi katika mechi hiyo.
Naye kiungo wa ushambuliaji wa Stars, Haruna Moshi 'Boban' aliyepewa mikoba ya Bocco huku Said Bahanunzi akipewa mikoba ya Samatta walisema kwamba wamekuja hapa kushinda.
"Tumekuja kushinda mechi hii kwa sababu ushindi ndiyo njia pekee itakayotuweka katika mazingira mazuri ya kujiandaa na mechi zilizoko mbele yetu," alisema Boban.
Kwa upande wake Bahanunzi alisema kwamba nafasi hiyo waliyoipata ya kusafiri umbali mrefu kuja kucheza mechi ya kirafiki ugenini ni changamoto kwao hivyo lazima washinde mechi hiyo.
Naye meneja wa timu hiyo Leopold Tasso Mukebezi alisema kwamba mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Molepolole uliopo umbali wa kilomita 60 kutoka katikati ya mjini wa Gaborone kuanzia saa 1:00 kwa saa za hapa na saa 2:00 kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi hapa Botswana, Nieman Kissasi, amesema kuwa Stars haiko peke yao hapa Botswana kwa sababu kuna Watanzania wengi wanaoishi hapa na kwamba watajitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo.
“Tumesikia ujio wa timu hii siku mbili zilizopita, tukaamua kujikusanya na kuandaa mikakati ya timu yetu kupata ushindi ikiwa ni pomoja na kuwatafutia hoteli nzuri ya kuishi, lakini pia tutakuja uwanjani kwa wingi kwa ajili ya kuwashangilia," alisema Kissasi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment