Monday, August 6, 2012

OSCAR APEWA JEZI NA.11 YA DIDIER DROGBA CHELSEA

Oscar akiwa kazini wakati wa mechi ya Brazil dhidi ya Belarus. katika michezo ya Olimpiki finayoendelea jijini London. Yosso huyu ndiye atakayetinga jezi za Drogba kuanzia msimu ujao.
Khaaaaa... yaani jezi yangu Na.11 nd'o mnampa huyu dogo Oscar?
LONDON, England
KLABU ya Chelsea imethibitisha leo hii kuwa mchezaji wao mpya, Oscar atavaa jezi Na.11 katika msimu ujao wa 2012-13 kufuatia Didier Drogba aliyekuwa akiivaa kuhamia klabu ya Shanghai Shenhua ya China.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil, ambaye hivi sasa anaichezea timu ya taifa lake katika michezo ya Olimpiki ya London 2012, atarithi jezi Na. 11 ya Drogba ambaye mchango wake katika Chelsea umemfanya achukuliwe kuwa ni mmoja wa wachezaji gwiji klabuni hapo, ikiwa ni baada ya kuisaidia kutwaa taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita.

Oscar alijiunga na Chelsea inayonolewa na kocha Roberto Di Matteo akitokea klabu ya Internacional ya Brazil mwezi uliopita kwa ada ya uhamisho inayotajwa kuwa ni paundi za England milioni 25 (Sh. bilioni 60) na atachuana kuwania namba katika kikosi cha kwanza cha na Eden Hazard ambaye ni mchezaji mpya kama yeye, Juan Mata, Florent Malouda na Daniel Sturridge.

Dogo huyo mwenye miaka 20, anafuata nyayo za wakali kama Damien Duff na Boudewijn Zenden, ambao wote waliivaa jezi Na.11 kabla haijatua kwa Drogba mwaka 2006.

Dennis Wise ni gwiji mwingine aliyewahi kuvaa jezi Na.11 ya Chelsea, akianza kuitumia mwaka 1993 wakati namba za wachezaji kikosini zilipoanza kutumika katika soka la England.

No comments:

Post a Comment