Tuesday, August 7, 2012

OKWI AKANUSHA KUFUZU MAJARIBIO

Okwi

KUMBE Emmanuel Okwi hakufanya majaribio hata siku moja na klabu ya Redbull Salzburg ya Austria, tofauti na ambavyo imekuwa ikitangazwa na uongozi wa Simba.

Viongozi wa Simba, wamekuwa wakisema mara kwa mara kuwa Okwi amefuzu majaribio hayo na kwamba wanatarajia kumuuza kwa euro 600,000 (sawa na Sh. bilioni 1.1) kama dili lake litafanikiwa.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Uganda amesema kuwa tangu alipotua Austria alikuwa mgonjwa hivyo hakufanya mazoezi hata siku moja.

Okwi amesema kutokana na kuugua, uongozi ulimueleza arejee nyumbani na hadi atakapoitwa tena.

Kauli hiyo inatia shaka ya kuwa pengine tayari kitumbua kimeshaingia mchanga na huenda yakajirudia yaliyotokea kwa Mrisho Ngassa alipoenda kufanyiwa majaribio West Ham United, ambapo alidai ataitwa tena kama ilivyomtokea tena wakati alipoenda kufanyiwa majaribio katika klabu ya Seattle Sounders FC ya Marekani.

Aidha, Okwi alikanusha mipango ya kujiunga na Yanga akisema ana mkataba.

"Nina mkataba na Simba na ninauheshimu, mkataba hauniruhusu kufanya mazungumzo na timu nyingine," alisema Okwi.

Yanga na Azam kwa nyakati tofauti zimehusishwa na mipango ya kutaka kumsajili mshambuliaji huyo mwenye kipaji kikubwa.

No comments:

Post a Comment