Tuesday, August 28, 2012

MOSES: NILIPAGAWA KUTAKIWA NA MABINGWA WA ULAYA CHELSEA

Winga wa kuingia nazo na mkali wa kuwapunguza mabeki, Victor Moses akipozi klabuni Chelsea baada ya kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Chelsea akitokea Wigan. Watu wako 'siriasi' kusaka mataji bhana...

VICTOR Moses amemhakikishia kocha Roberto Di Matteo kwamba yuko tayari kucheza nafasi yoyote uwanjani baada ya kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Chelsea uliogharimu paundi milioni 9 akitokea Wigan.

Moses alikuwa katika rada za Chelsea tangu alipong'aa mwishoni mwa msimu uliopita na kukisaidia kikosi cha Roberto Martinez kubaki katika Ligi Kuu ya England.

Na alikuwa katika kiwango cha juu kwa Wigan wakati wa kipigo chao cha 2-0 dhidi ya kikosi cha Di Matteo kwenye Uwanja wa DW katika mechi yao ya fungua pazia la Ligi Kuu ya England.

Hivi sasa baada ya kuthibitishwa kujiunga na klabu hiyo ya Stamford Bridge, anataka bosi wake kutambua kwamba kucheza mahala popote uwanjani.

Aliiambia tovuti ya klabu hiyo ya chelseafc.com: "Wakati nakua nilikuwa nikicheza kama beki wa kati lakini nikafikiria kwamba naweza kucheza mbele zaidi. Nilipoonwa kipaji changu cha Crystal Palace nilianza kucheza kama kiungo wa kati. Kisha nikaishia kucheza kama mshambuliaji, wingi ya kushoto, na ya kulia - kila mahala.

"Nilikwenda Wigan kucheza katika wingi ya kushoto zaidi lakini baadaye kocha akaona jinsi nilivyokuwa nikicheza na akawa akinitumia zaidi kulia. Msimu uliopita nilicheza zaidi kulia lakini wakati mwingine kushoto.

"Naweza pia kucheza kama mshambuliaji wa kati ama nyuma yake, naweza kucheza popote mbele. Najisikia huru kucheza popote kocha atakaponipanga."

Kiwango chake katika mechi dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa DW kilimshawishi Di Matteo, na mkurugenzi wa ufundi wa Chelsea, Michael Emanalo na mmiliki Roman Abramovich, kulipa kiasi walichotaka Wigan.

Moses alimfanya uchochoro beki wa kushoto wa Ashley Cole mara kadhaa na kocha wa Chelsea amesema kilichomvutia kwa nyota huyo mpya ni uwezo wake wa "kukokota ngoma".

Alisema: "Hicho ndicho kitu ninachokiweza zaidi, napenda kupokea mpira na kuanza kuwalamba chenga mabeki. Huwezi kupenda mabeki wakuchezee rafu kila mara unapokuwa na mpira, unahitaji kuwashughulisha, na hicho ndicho ninachokifanya.

"Sote tunajua Ashley Cole ni mmoja wa mabeki bora kabisa wa kushoto duniani na ni mchezaji anayedumu katika kiwango cha juu, hivyo ninapompita ninafurahi kwa sababu ni mchezaji mkubwa.

"Ninachopenda kuwaambia mashabiki ni kwamba wakae watulie, kuna mengi yanakuja kutoka kwa Victor Moses na ninatumai kuifanyia makubwa klabu hii na kuna mataji mengi yanakuja."

No comments:

Post a Comment