Thursday, August 23, 2012

KALALA JUNIOR ATAMBULISHWA TWANGA PEPETA

Mwanamuziki Kalala Junior akiimba mbele ya wanahabari wakati wa utambulisho wake wa kurejea katika bendi yake ya zamani ya African Stars 'Twanga Pepeta'
Mimi ni mwanamuziki niliyekamilika, hata gita napiga..... Mwanamuziki Kalala Junior akipiga gita mbele ya wanahabari wakati wa utambulisho wake wa kurejea katika bendi yake ya zamani ya African Stars 'Twanga Pepeta'

Na drums pia nazidunda kisawa sawa... Mwanamuziki Kalala Junior akipiga drums mbele ya wanahabari wakati wa utambulisho wake wa kurejea katika bendi yake ya zamani ya African Stars 'Twanga Pepeta'

Muimbaji wa Twanga Pepeta, Saleh Kupaza akiimba mbele ya wanahabari wakati wa utambulisho wake wa kurejea katika bendi yake ya zamani ya African Stars 'Twanga Pepeta'


BAADA ya kuikacha bendi ya Mapacha Watatu aliyoiasisi pamoja na wenzake wawili, muimbaji na rapa maarufu nchini Kalala Junior amerejea katika bendi yake ya zamani ya African Stars 'Twanga Pepeta' na tayari ametambulishwa leo hii.

Kalala aliondoka Twanga na kwenda kuanzisha bendi mpya ya MAPACHA WANNE akiwa pamoja na Jose Mara kutoka FM Academia, Khalid Chokoraa 'Nywele Ngumu' kutoka Twanga Pepeta na Chaz Baba kutoka Twanga pia lakini Chaz alijitoa kabla bendi hiyo haijazinduliwa na kurejea Twanga na kusababisha watatu waliobaki kubadili jina na kuiita MAPACHA WATATU. Hata hivyo, Chaz Baba naye aliondoka baadaye Twanga na kutua Mashujaa Band, ambako amepewa urais wa bendi hiyo.

Baada ya kuitumikia kwa muda naye akiwa mmoja wa wakurugenzi watatu wa MAPACHA WATATU, Kalala alitangaza kujiondoa katika bendi hiyo baada ya kutofautiana msimamo na wenzake.

Wakati akitambulishwa kurejea Twanga jijini Dar es Salaam leo, Kalala, ambaye alikuwa ameambatana na baba yake mzazi ambaye pia ni mwanamuziki gwiji nchini Hamza Kalala 'Komandoo', alisema daima Twanga ni nyumbani kwake na hakika Twanga ni kisima cha burudani.

Kisha alithibitisha mbele ya wanahabari namna alivyo mwanamuziki aliyekamilika pale alipoimba, aliporap, kucheza, kupiga gita na pia drums.

Kalala ataanza kazi rasmi Twanga Pepeta Agosti 31.

No comments:

Post a Comment