Friday, August 10, 2012

DI MARIA ASAINI MKATABA MPYA UTAKAOMBAKIZA REAL MADRID HADI 2018

Di Maria
Di Maria
MADRID, Hispania
Real Madrid wamefikia makubaliano na Angel Di Maria ya kuongeza mkataba kwa miaka sita zaidi, hivyo kumfanya straika huyo abaki klabuni hapo hadi mwishoni mwa msimu wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania 2017-18.

Mkataba mpya wa straika huyo mwenye miaka 24 utamalizika Juni 30, 2018, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kupitia tovuti rasmi ya klabu hiyo. Hata hivyo, nyongeza ya maslahi itokanayo na mkataba huo mpya haikuwekwa wazi.

Hii ni hatua nyingine kubwa ya mabadiliko katika mkataba wa Di Maria ndani ya kipindi cha miezi miwili baada ya straika huyo wa kimataifa wa Argentina kuongezwa mshahara Juni, ambao ulipanda kutoka euro milioni 2 (Sh. bilioni 3.8) hadi euro milioni 3 (Sh. bilioni 5.7) kwa mwaka.

Di Maria amelezea furaha yake baada ya kuongezewa mkataba, akiiambia Marca: "Nimefurahi sana kwa sababu najua kwamba klabu imeniongezea mkataba kutokana na kiwango ninachoonyesha. Najihisi kuungwa mkono sana na kupendwa na klabu na mashabiki."

"Binafsi, nimeimarika sana, shukrani kwa Mourinho. Namshukuru Mungu kwa mazoezi na kujituma kwangu kila siku, na katika kila mechi, nimefanikiwa kujitengenezea wapenzi kutoka kwa mashabiki. Nafurahishwa sana nao."

"Natimiza ndoto ambayo nilikuwa nayo tangu utotoni. Nina furaha sana hapa na kuongezwa kwa mkataba wangu kunanipa fursa ya kubaki kwa miaka mingi na kuendelea kukomaa."

Di Maria alijiunga Real Madrid akitokea Benfica Juni 2010 na tangu wakati huo ameichezea klabu hiyo mara 83, akiibuka kuwa mmoja wa wachezaji muhimu waliosaidia kupatikana kwa ubingwa wa La Liga msimu uliopita wa 2011-12.

No comments:

Post a Comment