Saturday, August 4, 2012

BOLT ATINGA NUSU FAINALI MITA 100 OLIMPIKI

*Ashinda kundi lake kwa kutumia sekunde 10.09, Blake ashinda lake kwa 10.00

Bolt akishinda mita 100 leo
BINGWA mtetezi wa Olimpiki, Usain Bolt ametinga kirahisi nusu fainali ya mbio za mita 100 katika mchuano wa mchujo uliomalizika hivi punde katika Michezo ya Olimpiki ya London 2012.

Mjamaicha huyo alisema alianza vibaya lakini akarejea kuwa vyema na kumaliza wa kwanza katika kundi lake la mchujo kwenye Uwanja wa Olimpiki jijini London akitumia sekunde 10.09.

Mmarekani Ryan Bailey ndiye aliyekimbia kwa kasi zaidi ya wote katika mbio hizo za mchujo baada ya kushinda kundi lake kwa kutumia sekunde 9.88.

Yosso Muingereza Adam Gemili alimaliza wa pili nyuma ya Powell, katika kundi lao huku Muingereza mwingine Dwain Chambers akishinda katika kundi lake kati ya makundi saba ya mchujo kwa kutumia sekunde 10.02, muda ambao ni moja ya aliyopata kukimbia kwa kasi zaidi katika historia yake ya mchezo huo.


Muingereza mwenzake James Desaolu pia alifuzu, kwani washindi watatu kutoka kila kundi kati ya makundi saba ya mchujo yaliyokuwapo, walifuzu moja kwa moja pamoja na "best luza" wawili ambao watakimbia pia nusu fainali zitakazofanyika kesho.

Bolt aliiambia BBC Sport: "Nilitarajia mapokezi mazuri London na na nilijiandaa. Nilianza vibaya lakini nina furaha kwamba jambo hilo limenitokea sasa sio katika fainali."

Gemili (18), ambaye ni hivi karibuni tu ndio amejiunga na mchezo wa riadha akitokea kucheza soka, alisema baada ya kutumia muda wa sekunde 10.11: "Kuingia katika Olimpiki na kutembea uwanjani huku unashangiliwa ni kama inatokea ndotoni mwangu. Mambo haya yametokea haraka sana ndani ya mwaka huu, lakini nimefanya kazi kwa bidii. Nimejiunga na mchezo wa riadha Januari tu matokeo yanaonekana sasa.

"Ni lazima umheshimu Asafa Powell, lakini hupaswi kumheshimu mpinzani wako kupindukia. Yeye ni mtu wa matawi mengine. Nimekimbia vizuri na ninafurahia hilo."

Chambers, ameweza kushindana kwenye Olimpiki baada ya Mahakama ya Upatanishi wa Kimichezo kutengua hukumu yake ya kifungo cha maisha kwa kutumia dawa zinazokatazwa michezoni, alikiri hofu kabla ya mchuano.

"Ninafuraha kufuzu kutokea kwenye mchujo, sapoti ya mashabiki ilikuwa nzuri," alisema Chambers. "Ilinihamasisha na ninaona namna ambavyo imetoa mchango kwa watu kama Jess.

"Unaweza kufanya mazoezi mwaka mzima lakini la muhimu unatakiwa kukimbia vyema kwenye mashindano na nimekuwa nikichukua hatua kwa hatu kufikia hapa. Nina furaha sana kuwa hapa. Ni mashindano ya kasi na ninahitaji kusonga mbele."

Katika jambo la kushangaza, bingwa wa zamani wa dunia, Kim Collins alitemwa kwenye mashindano hayo baada ya kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu kutokana na kukiuka taratibu na kuondoka katika Kijiji cha Wanamichezo.

Aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: "Mashabiki wangu. Siwezi kusema uongo. Sitakimbia leo baadaye. Hata watu walio magerezani hutembelewa na wake zao."

No comments:

Post a Comment