Wednesday, August 29, 2012

AKUFFOR, NGASSA WATISHA SIMBA IKIIZAMISHA JKT OLJORO 2-1

Nyota wapya wa Simba, Patrick Ochieng (kushoto) na Daniel Akuffor wakipozi kwa picha.

SIMBA imepata ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha katika mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid leo jioni huku magoli yote matatu yakisababishwa na nyota wapya waliojiunga na klabu hiyo ya Msimbazi katika kipindi hiki cha usajili.

Magoli mawili ya Simba yamefungwa na Mghana Daniel Akuffor na Mrisho Ngassa wakati la wenyeji limesababishwa na beki mpya wa mabingwa hao wa Tanzania Bara, Pascal Ochieng, aliyemchezea madhambi mchezaji wa Oljoro ndani ya 18.

Akuffor aliyejiunga akitokea Stella Abidjan ya Ivory Coast, aliifungia Simba goli la kuongoza katika ya 28 kufuatia pasi ya Ngassa na Ngassa, aliyetua Msimbazi kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea Azam FC, alifunga la pili katika dakika ya 76 akimalizia pasi ya nyota mwingine mpya Abdallah Juma, aliyeingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Akuffor.

Ochieng ambaye alilazimika kuununua mkataba wake wa miezi sita na klabu ya AFC Leopards, alisababisha penalti iliyofungwa na Markus Raphael na kuwapa Oljoro goli la kufutia machozi dakika moja kabla ya mechi kumalizika.

Kocha Milovan Cirkovic alikifanyia mabadiliko kikosi chake kilichoshinda 2-1 dhidi ya Mathare United ambapo aliwaanzishia benchi Haruna Moshi 'Boban', Amir Maftah, Nassoro Said 'Chollo', Abdalla Juma na Salum Kinje na nafasi zao kuwaanzisha Haruna Shamte, Paul Ngalema, Amri Kiemba, Ngassa na Ramadhani Chombo 'Redondo'. 

Simba Jumapili itacheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Nairobi City Stars ya Kenya, ambayo iliwaharibia sherehe zao za Simba Day Agosti 8, 2012 kwa kuwapa kichapo cha 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

Vikosi vilikuwa; Simba: Wilbert Mweta, Haruna Shamte, Paul Ngalema, Pascal Ochieng, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba/ Salim Kinje (dk.46), Ramadhani Chombo 'Redondo', Daniel Akuffor/ Abdallah Juma (dk. 46), Mrisho Ngassa na Kigi Makasi/ Uhuru Selemani (dk. 46).

JKT Oljoro: Shaibu Issa, Yassin Juma, Napho Zubery, Marcus Raphael, Salum Mbonde, Emmanuel Memba, Karage Mgunda, Meshack Nyambele, Amir Hamad, Ibrahim Mamba na Sixbeth Mohammed/ Hamis Saleh (dk. 46).

Wakati huo huo, Ochieng amelazimika kuununua mkataba wake na AFC Leopards ili kupata kibali cha uhamisho wake wa kujiunga na Simba, taarifa iliyotumwa jana katika tovuti ya klabu hiyo ya Kenya ilisema.

Ochieng, beki wa kati ambaye hakuwa na furaha Leopards alijiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miezi sita katikati ya msimu akitokea katika klabu yenye matatizo ya kifedha ya Rangers FC.

Taarifa ya tovuti ya AFC ilisema jana kuwa Ochieng anaondoka katika klabu hiyo akiwa hajacheza mechi hata moja ya kimashindano na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyekaa klabuni hapo kwa muda mfupi usiozidi wiki tano.

Katibu Mkuu wa Leopards, Winston Kitui alithibitisha kwenye tovuti hiyo kuwa Ochieng ameununua mkataba wake, na kuifungulia njia klabu hiyo kuruhusu kutolewa kwa kibali chake cha uhamisho wa kimataifa (ITC) kutua Simba.

“Tumemuagiza meneja wetu wa ITC kukamilisha jambo hilo,” alisema.

Ufafanuzi huo unahitimisha utata uliozunguka hatima ya beki huyo uliokuwapo kwa klabu zote mbili.

Wakati Leopards ilikanusha kufahamu chochote kuhusu mazungumzo ya uhamisho wa mchezaji huyo, Simba ilikuwa ikikaririwa na vyombo vya habari za Tanzania na mitandao ya kijamii kwamba imemsajili Ochieng.

Kitui alisema Leopards imeafiki mchezaji huyo kuununua mkataba wake baada ya kuruhusiwa na kocha Jan Koops ambaye alisema kwamba hayuko tayari kumchezesha mchezaji ambaye mawazo yake yako katika klabu nyingine.

Vyanzo pia vilisema kwamba Ochieng hakuwa na raha baada ya kubaini kwamba kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Leopards ilikuwa ni jambo gumu kwa kuzingatia kwamba wapinzani wake katika nafasi ya ulinzi wa kati, Eric Masika na Nahimana Jonas, wako katika kiwango cha juu kisichohitaji maswali.

Katika kipindi chake kifupi klabu hapo, alicheza mechi moja tu ya kirafiki ambayo alishindwa kuonyesha kiwango.

“Bado tunamtakia mafanikio mema aendako,” alisema Kitui.

Mjumbe wa kamati ya utendaji ya AFC Leopards, Richard Ekelye, alisema pamoja na Ochieng, walimalizana pia na Salim Kinje baada ya Simba kutoa pesa walizohitaji. Hata hivyo hakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha kilicholipwa na Simba kwa ajili ya nyota hao wawili.
 
Ochieng na Kinje wanaendelea kuitumikia klabu yao mpya ya Simba mjini Arusha wakati wakisubiri kuwasili kwa ITC zao.

No comments:

Post a Comment