Monday, July 30, 2012

WABUNGE FREEMAN MBOWE, STEVEN WASIRA WATAKIWA KUCHAPANA MAKONDE JUKWAANI KAMA WEMA NA WOLPER


*WENGINE WANAOTAKIWA KUONYESHANA UBAVU NI HALIMA MDEE Vs JOB NDUGAI, JOSHUA NASSARI Vs LIVINGSTONE LUSINDE, DK. MARY NAGU Vs ROSE KAMILI

Cheki mkono huu... Mhe. Mbowe anatakiwa kupimana ubavu na Mhe. Wassira. Itakuwaje?
Mhe. Wassira a.k.a Tyson anatakiwa kuchapana makonde na Mhe. Mbowe. Si unamcheki anavyoonekana fiti?
Mhe. Ndugai... pamoja na cheko hili, bado anatakiwa eti achapane makonde na Mhe. Halima Mdee. Ni haki kweli?

Mhe. Halima Mdee... pamoja na kuwa kamanda mwenye muonekano wa kuvutia, lakini anatakiwa awe ngangari kama akina Wema Sepetu ili amtoe nishai bosi wake bungeni, Mhe. Ndugai. Je, ataweza lakini?
Mhe Nassari... huyu mshkaji anayefahamika pia kama Dogo Janja hasimu wake, Mhe. Lusinde a.k.a Kibajaji walichambana sana wakati wa uchaguzi mdogo kule Arumeru Mashariki. Sasa anatakiwa kumalizana na Kibajaji kwa mangumi makali jukwaani. Patachimbika ile mbaya, sivyo? 
Huyu nd'o Mhe. Lusinde mwenyewe... aliibua mjadala kutokana na mineno yake mikali wakati wa uchaguzi mdogo kule Aumeru Mashariki. Msela huyu wa Mtera sasa anatakiwa kuchapana makonde kavukavu na Mhe. Nassari 'Dogo Janja'. Itakuwa safi eenhhh... mi simo!
Wema Sepetu (kushoto) na Jacqueline Wolper wakipongezana baada ya kumaliza pambano lao la ngumi hivi karibuni.
Wabunge wamemuomba Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai abariki pambano kali la ngumi baina ya wabunge kadhaa wakiwemo Mbunge wa Jimbo la Hai na kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe, ambaye ametakiwa kuchapana makonde mbele ya hadhara na Mbunge wa Jimbo la Bunda (CCM) ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mhe. Stephen Wassira.

Akizungumza bungeni jioni hii kabla ya kuahirisha kikao cha leo, Mhe. Ndugai alisema kwamba amepokea maombi kadhaa kutoka kwa wabunge yanayopendekeza kuwepo kwa mpambano wa ngumi baina ya wabunge wakati wa Tamasha la Matumaini litakalofanyika kwenye Uwanaja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mbali na pendekezo la kuwepo kwa pambano la Mbowe na Wassira ambalo lilishangiliwa sana bungeni, Mhe. Ndugai alitaja mapendekezo mengine aliyopokea kupitia ujumbe mfupi uliotumwa na wabunge mbalimbali kuwa ni kati ya yeye (Ndugai) aliyetakiwa kupimana ubavu na Mbunge wa Kawe (CHADEMA), Mhe. Halima Mdee.

Mapambano mengine yaliyopendekezwa siku hiyo ni kati ya Mbunge wa Jimbo la Hanang (CCM) ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dk. Mary Nagu na Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Mhe. Rose Kamili.

Wengine waliotakiwa kuchapana makonde katika tamasha hilo ni Mbunge wa Arumeru Mashariki (CHADEMA), Mhe. Joshua Nassari  ambaye anatakiwa kupimana ubavu na Mbunge wa Jimbo la Mtera (CCM), Mhe. Livistone Lusinde.

Baada ya orodha hiyo kutangazwa na Naibu Spika, wabunge karibu wote waliangua kicheko huku wakishikilia mbavu zao. Kisha kikao cha leo kikaahirishwa hadi kesho saa 3:00 asubuhi.
 
Katika tamasha kama hilo (la matumaini) lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, waigizaji wa kike nyota nchini, Wema Sepetu na Jacqueline Wolper walipanda ulingoni na kupigana kwa raundi mbili. Matokeo yalikuwa sare na waigizaji hao waliowahi kuripotiwa kuwa wana ‘bifu’ kali kati yao walishikana mikono na kukumbatiana, ikiwa ni ishara ya kuwepo kwa maelewano baina yao.

No comments:

Post a Comment