Tuesday, July 17, 2012

VAN PERSIE AREJEA MAZOEZINI ARSENAL

Robin van Persie akiwa mazoezini na wachezaji wenzake wa Arsenal.

LONDON, Uingereza
ROBIN van Persie amerejea mazoezini na klabu ya Arsenal juzi huku akisisitiza kwamba bado anataka kuondoka.

Na inaonekana kwamba Arsenal wameshabwaga manyanga kwa nahodha wao huyo kwani "katalogi" mpya ya kwenye internet haijamjumuisha.

Hivi sasa, Mholanzi huyo mwenye thamani ya paundi milioni 30 anataka mazungumzo mapya na kocha Arsene Wenger na mkurugenzi mtendaji Ivan Gazidis.

Van Persie (28), anataka hatma yake ifahamike kabla kikosi hakijaondoka kwenda Mashariki ya Mbali Jumamosi.

Msemaji wa Arsenal alithibitisha: "Robin alirejea mazoezini Jumatatu kama ilivyotarajiwa na ameweka wazi kwamba anataka kuondoka na kujua hatma yake mapema iwezekanavyo.

"Hakuna tarehe iliyoafikiwa ya mkutano huo."

Van Persie, ambaye ana mwaka mmoja umebaki katika mkataba wake na Arsenal, anatakiwa na Man City, Man United, Juventus na Real Madrid.

Lakini mfungaji bora huyo wa msimu uliopita wa Ligi Kuu ya England kutokana na magoli yake 30, hajajumuishwa kwenye picha ya pamoja ya wachezaji kwa ajili ya kuwekwa kwenye mtandao.

Van Persie alisaidia uzinduzi wa jezi mpya za Arsenal watakazozaa katika mechi za nyumbani Aprili lakini hajawekwa katika picha za vipeperushi vilivyowekwa kwenye mtandao, ambayo zinaonyesha jezi mpya za rangi ya zambarau watakazozitumia katika mechi zao za ugenini.

RVP anataka kuondoka Arsenal kwa ajili ya kusaka timu zinazopigania makombe, lakini kama suala lake halitaafikiwa hadi wikiendi, atalazimika kuambatana na timu katika ziara ya kujiandaa na msimu mpya ya Mashariki ya Mbali.

No comments:

Post a Comment