Monday, July 9, 2012

UWANJA MBOVU WAMTOA MADONDA KOCHA SAINTFIET YANGA

Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet (kushoto) akimwonyesha daktari wa timu hiyo, Juma Sufian eneo alilochubuka wakati wa mazoezi kwenye uwanja uliojaa vipara wa Bora Kijitonyama jijini Dar es Salaam muda mfupi uliopita. Picha: Sanula Athanas

Na Sanula Athanas
KAMA alidhani hapa ni Ulaya, kocha mpya wa Yanga, Tom Saintfiet atakuwa anakosea sana. Hapa ndio Bongo bhana!


Mzungu wa Yanga leo asubuhi amejikuta akichubuka katika maeneo mbalimbali ya mwili wake kutokana na timu hiyo kubwa nchini kutokuwa na uwanja wake wa kisasa wa mazoezi na kulazimika kutumia viwanja vya kukodi vilivyojaa vipara.


Mbelgiji huyo ambaye huwaonyesha wachezaji wake kwa vitendo kila zoezi analowapa, alijikuta akichubuka katika maeneo mbalimbali ya mwili kufuatia mazoezi yake yakiwamo ya kulala chini kifudifudi na "kusimamia" tumbo huku mikono na miguu vikiwa juu.


"Tafadhalini msinipige picha maana nguo yangu imechafuka sana," alisema kocha huyo huku akishika maeneo ya mwili wake kama kwenye mikono na magoti na miguuni akionyesha kuugulia huku mwili wake ukiwa umeiva na kuwa mwekundu. STRAIKA, hata hivyo, ilikuwa imeshapata picha kabla hajaomba kutopigwa picha.


"Uwanja huu ni mbaya sana. Kuna wachezaji hapa ambao wangeweza kuja kucheza kama Messi na Ronaldo lakini kwa uwanja kama huu hawawezi kwa sababu kuna maeneo mpira ukiupiga unahama ulipotaka kuupeleka," alisema Saintfiet aliyesaini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha klabu hiyo ya Jangwani.


Mabingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga, wanaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Bora uliopo Kijitonyama jijini Dar es Saalam kujiandaa kutetea taji lao katika michuano hiyo itakayoanza Julai 14. 

No comments:

Post a Comment