Saturday, July 7, 2012

SUNZUUU.... SIMBA YAMALIZA KILELENI

Na Somoe Ng'itu, Zanzibar
GOLI pekee la kichwa kutoka kwa straika Mzambia Felix Sunzu lilitosha kuwapeleka mabingwa wa soka wa Tanzania Bara, Simba, katika nusu fainali ya michuano ya Kombe la Urafiki inayoendelea mjini hapa kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya timu ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 23 ya Zanzibar, Karume Boys. 

Vijana wa Zanzibar walijitahidi kucheza vyema lakini, Sunzu aliwathibitishia kuwa yeye ni mkubwa kwao wakati alipofungwa kwa kichwa katika dakika ya 58 na kuifanya Simba imalize ikiwa kileleni mwa kundi kutokana na kufikisha pointi 7 baada ya mechi tatu. Imeshinda mbili na kutoka sare moja dhidi ya Azam FC.

Simba ilianza vyema michuano hiyo inayofanyika kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa kwa ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya mabingwa wa Zanzibar, Mafunzo kabla ya kuja kushikiliwa kwa sare ya 1-1 na Azam, ambao ni washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Bara.

Azam FC ilimaliza ikiwa ya pili kwa kuwa na pointi 5 baada ya sare mbili na ushindi katika mechi iliyochezwa mapema jana.

Katika mechi hiyo, Azam iliilaza Mafunzo ya hapa kwa mabao 3-2.

Hadi mapumziko, Azam waliongoza kwa magoli 2-0 kupitia kwa Ramadhani Chombo "Redondo" na Kipre Tchetche.

Hata hivyo, dakika ya kwanza baada ya mapumziko, wenyeji walipata bao la kwanza kupitia kwa Sadick na wakaongeza la pili katika dakika ya 62 kupitia kwa Mohammed Abdulrahman na kufanya ngoma kuwa 2-2.

Zikiwa zimesalia dakika 8 mchezo kumalizika, Ibrahim Mwaipopo aliifungia Azam bao 3 lililoifanya Azam kufikisha pointi tano baada ya mechi tatu.

Katika mechi ya kwanza, Azam walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Karume Boys (U23) ya Zanzibar kabla ya kutoka sare nyingine ya 1-1 dhidi ya Simba.

No comments:

Post a Comment