Wednesday, July 18, 2012

SIMBA NI MIUJIZA TU NDO' ITAWAZUIA KWENDA ROBO FAINALI

Kiungo wa Simba, Amri Kiemba (18) akiwania mpira dhidi ya kipa wa Ports ya Djibout, Kalid Moursal (wa pili kushoto) wakati wa mechi yao ya pili ya Kundi A la michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (kombe la Kagame) 2012 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

Na Mwandishi Wetu
SIMBA imeingiza mguu mmoja katika robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, kufuatia ushindi wa 3-0, dhidi ya timu dhaifu ya Ports ya Djibout, ambayo sasa imefungwa jumla ya mabao 10-0 katika mechi zao mbili za Kundi A.


Ports ilifungwa 7-0 dhidi ya Vita Club ya DRC katika mechi yao ya kwanza kwenye uwanja wa Chamazi Jumapili na mashabiki wa Simba leo walitarajia ushindi ambao haukupatikana kirahisi.


Mashabiki wa Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambao waliamini timu yao ingeibuka na ushindi mnono wa kujibu kulichofanywa na mahasimu wao Yanga jana, ambao walishinda 7-1 dhidi ya Wau Salaam, walianza kupandwa na presha wakati timu hizo zilipoenda mapumziko matokeo yakiwa bado ni 0-0.


Wekundu walilazimika kusubiri hadi baada ya saa nzima ili kupata goli la kwanza lililofungwa na mshambuliaji wao mpya Abdallah Juma kufuatia krosi ya Mwinyi Kazimoto.


Mzambia Felix Sunzu aliongeza la pili kwa njia ya penalti baada ya beki wa Ports kuzuia "kanzu' kwa mkono akiwa ndani ya boksi.


Abdallah Juma, aliyeingia katika dakika ya kwanza ya kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Amri Kiemba, alikosa nafasi ya wazi akiwa jirani na lango tupu baada ya kipa kupigwa chenga katika dakika ya 68 na kujinyima fursa ya kuwa mchezaji wa pili kufunga 'hat trick' katika michuano ya mwaka huu baada ya Hamis Kiiza wa Yanga.


Juma alirekebisha makosa yake katika dakika ya 73 kwa kufunga goli "tamu' la kichwa kufuatia krosi ya Mwinyi Kazimoto na kuipa Simba pointi tatu za kwanza baada ya kuanza michuano vibaya kwa kipigo cha 2-0 kutoka kwa URA ya Uganda.


URA ambayo tayari imethibitisha kuwa ni timu ya kuogopa msimu huu, imetinga robo fainali kutokana na kuwa pointi sita baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya timu ngumu ya Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mechi nyingine ya Kundi A iliyochezwa mapema leo saa 8:00 mchana.


Simba inaendelea kubaki katika nafasi ya tatu ya kundi lao kutokana na kuwa pointi 3 sawa na Vita Club itakayokumbana nayo Jumamosi, ambayo iko katika nafasi ya pili kutokana na kuwa na wastani mzuri wa magoli.


Michuano hiyo itaendelea kesho ambapo Atletico ya Burundi yenye pointi 4 itacheza dhidi Wau Saalam (ambayo haina pointi) katika mechi yao ya mwisho ya Kundi C linaloijumuisha Yanga, kabla ya jioni wawakilishi wa Zanzibar, Mafunzo kuivaa Tusker ya Kenya katika Kundi B.


Katika mechi ya Simba kikosi kilikuwa: Juma Kaseja, Haruna Shamte/ Juma Nyosso (dk. 46), Amir Maftah, Shomari Kapombe, Lino Masombo, Mussa Mudde, Kanu Mbiyavanga, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba/ Abdallah Juma (dk.46), Haruna Moshi 'Boban'/ Uhuru Selemani (dk. 70), Felix Sunzu. 

No comments:

Post a Comment