Wednesday, July 18, 2012

KATIBU TFF AWASHUKIA VIONGOZI SIMBA


Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, amewataka viongozi wa Simba na klabu nyingine nchini kuacha tabia ya kujisafisha kwa wanachama wao kwa kutupia mzigo wa lawama shirikisho hilo pindi wanapoteleza kwa kufanya mambo kinyume cha utaratibu.

Akizungumza leo katika mahojiano yake na kituo kimoja cha luninga kuhusiana na utata wa beki Kevin Yondani aliyeikacha Simba na kuichezea Yanga katika michuano inayoendelea ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame),  katibu huyo alisema kuwa kuna makosa yamefanywa na uongozi wa Simba kuhusiana na mkataba wa mchezaji huyo; na kwamba sasa wanachofanya ni kuwatupia mzigo TFF.

“Siasa za kutupia mzigo TFF zimepitwa na wakati,” alisema Angetile na kutaka viongozi wa klabu waache tabia hiyo.

Akifafanua, Angetile alisema kuwa mkataba wa awali wa Yondani na klabu ya Simba ulimalizika Mei 31, 2012, na kwa mujibu wa kanuni, mkataba mwingine wa kumuongezea Yondani ulipaswa kuonyesha kuwa unaanzia katika kipindi cha kabla ya kumalizika kwa mkataba wa awali, akitolea mfano Mei 29.

Hata hivyo, akasema kuwa mkataba mwingine unaolalamikiwa na Simba kuwa ndio uliomuongezea Yondani kipindi cha kubaki klabuni kwao unaonyesha kuwa unaanzia Juni 1, 2012, jambo ambalo si sahihi kwani tarehe hiyo inaashiria kuwa huo sasa ni mkataba mpya.
Katibu huyo aliongeza kuwa kasoro nyingine za mkataba unaolalamikiwa na viongozi wa Simba ni pamoja na tarehe ya kusainiwa kwake, ambapo unaonyesha kuwa uliingiwa Desemba 23, 2012.

“Hili nalo ni tatizo kwa sababu siku hiyo bado haijafikiwa,” alisema Angetile.
Akaongeza kuwa kwa sababu hiyo, wao (TFF) hawawezi kumzuia Yondani kuichezea Yanga katika michuano ya Kagame kwa mkataba wa Simba ambao ni “controversial” (wenye utata).
Akijibu tuhuma kwamba kuna maamuzi yaliyofanywa kwa kutegemea uamuzi wake binafsi, Angetile alisema kuwa hilo kamwe haliwezekani kwani TFF ni taasisi.

“Hii (TFF) ni taasisi. Mtu huwezi kufanya maamuzi peke yako,” alisema, kabla ya kueleza zaidi kuwa suala la kuongeza mkataba wa wachezaji (kama Yondani) liko katika mamlaka ya katibu na hivyo hawakuwa tayari kutumia “controversial documents” (nyaraka zenye utata) kumzuia Yondani asicheze Kagame.

Angetile alisisitiza kuwa kuwa enzi za kufungia wachezaji zimeshapita kwani hivi sasa jukumu la kusajili liko kwa klabu zenyewe.

SOMO LA FIGO KUTOKA BARCA KWENDA REAL

Katika hatua nyingine, Angetile alizitaka klabu za soka nchini kusajili kwa kuzingatia vigezo vya kitaalam na kuweka kando ushabiki na siasa, huku pia akizishauri kubadilika na kuiacha kugombania wachezaji.

Akashauri kwamba badala ya kutumia muda mwingi kulumbana, klabu zikae na kuzungumza juu ya kuuziana wachezaji wanaoonyesha dhamira ya kutaka kuhamia timu nyingine.

Katibu huyo alihoji kuwa, kama iliwezekana kwa straika Luis Figo kuihama Barcelona na kwenda kwa mahasimu wao wa jadi Real Madrid, kwanini ishindikane kwa wachezaji wa klabu za hapa nchini kuuziana wachezaji bila kuzozana?

“Cha muhimu ni klabu yenye mchezaji kutaja bei yao,” alisema Angetile.

No comments:

Post a Comment