Thursday, July 19, 2012

MPOKI WA ORIJINO COMEDY AJISIFU KWA ‘UMATEMATE’


ADAI BARNABA HANA KITU, HAWEZI KUMTOZA KWA VIDEO ALIYOMSHIRIKISHA WIMBO ‘MAGUBEGUBE’

Mpoki (wa pili kulia) akiwa na wasanii wenzake wa kundi la Orijino Comedy.

Mpoki (kulia) akiwa na nyota wa bongoflvea, Barnaba.
Na Sanula Athanas
Msanii nyota wa vichekesho nchini, Sylivester Mjuni ‘Mpoki’, amesema kuwa yeye hujiingizia fedha nyingi kupitia fani yake na hivyo hana sababu ya kumtoza hela msanii yeyote wa muziki wa bongofleva anayetaka kushirikiana naye kurekodi nyimbo zake.

“Nimekuwa nikishirikishwa na wasanii wengi tu wa ‘Bongo’ lakini siwatozi chochote maana hawana mshiko wa kutosha, leo nimwambie Barnaba anilipe Sh. Milioni 50 kutokana na ushiriki wangu kwenye wimbo wake wa ‘Magubegube’ nitakuwa ninamkomoa, siku zote nashirikiana nao ili kuwainua, kama kuna msanii amenilipa pesa aje hapa,” amejigamba Mpoki.

“Situngi nyimbo kwa nia ya kujipatia pesa bali nafanya hivyo ili kuburudisha mashabiki wangu. Mimi nina kazi yangu nzuri ambayo mnaijua, inaniingizia pesa nyingi, hivyo ni kheri nikatenga kiasi kidogo ninachokipata kutokana na kazi hiyo kuingia studio na kurekodi nyimbo kuwaburudisha watu,” amesema Mpoki.

Wakati wasanii nchini wakiumiza vichwa vyao kutunga nyimbo ili kujipatia fedha, Mpoki ametoa mpya baada ya kueleza kuwa hatungi nyimbo kwa kusaka pesa bali kufurahisha mashabiki wake.

Mpoki ameyasema yote hayo jana asubuhi wakati akihojiwa na watangazaji wa kipndi cha ‘Leo Tena’ kinachorushwa na kituo cha redio ya Clouds FM na kutambulisha wimbo wake mpya alioupa jina la ‘Mademu wa Kibongo’.

Msanii huyo wa kundi la Orijino Comedy, amesema halipwi chochote na wasanii kutoka nchini ambao wamekuwa wakimshirikisha kwenye nyimbo zao kwa kuwa kipato chao kiko chini.

Katika wimbo huo, Mpoki anayesifika kwa misemo mikali na ya kuchekesha, anaeleza sifa za wanawake wanaoishi katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Awali mtayarishaji wake, Lamar ambaye alikuwa ameambatana naye, aliweka wazi juu ya usumbufu anaopata katika kuandaa nyimbo za Mpoki, akisema kwamba ni mtu wa kuchekesha kila mahala kiasi kwamba hata waingiapo studio, wakati mwingine hujikuta wakiishia kucheka tu badala ya kufanya kazi.

No comments:

Post a Comment