Tuesday, July 10, 2012

MJINI MAGHARIBI WAMWAGA VILIO TEMEKE WAKITINGA NUSU FAINALI COPA COCA COLA

Kiungo wa timu ya soka ya Temeke, Bakari Ntalunkundo akishangilia baada ya kufunga goli la dakika za majeruhi na kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Mjini Magharibi katika mechi ya robo fainali ya michuano ya Copa Copa Cola kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume leo asubuhi. Goli hilo lililazimisha mechi kuingia katika hatua ya kupigiana matuta na Temeke ikashinda kwa penalti 4-2 na kutinga nusu fainali.Picha: Sanula Athanas

Ni zamu ya matuta sasa. Picha: Sanula Athanas

Kipa wa Temeke, Shukuru Mohammed (kushoto) akishuhudia mpira wa penalti iliyopigwa na Allan Kombo wa timu ya Mjini Magharibi wakati wa kupigiana matuta. Picha: Sanula Atahans



Na Sanula Athanas
PENALTI zifutwe! Wachezaji na viongozi wa timu ya Mjini Magharibi walijikuta wakiangua vilio baada ya timu yao kutolewa kwenye mashindano yanayoendelea ya Copa Cocacola baada ya kupoteza mechi yao ya robo fainali dhidi ya Temeke kwa penalti 4-2 jana asubuhi baada ya dakika 90 za mechi hiyo kumalizika kwa sare ya goli 1-1 kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.


NIPASHE lilishuhudia wachezaji na viongozi wa timu hiyo wakiangua vilio baada ya kushindwa kulinda goli moja walilolipata kupitia kwa mshambuliaji Salum Songoro katika dakika ya 79 na kujikuta wakilazimishwa kuingia kwenye hatua ya matuta baada ya kiungo wa Temeke, Bakari Ntalukumbo kuipatia timu yake goli la kusawazisha katika dakika ya mwisho ya dakika 2 zilizoongezwa.


Anuari Kilemile alikosa penalti upande wa Temeke wakati Abraham Saidi na Salum Songoro (aliyefunga goli) wakikosa upande wa Mjini Magharibi na penalti ya tano kwa Mjini Magharibi haikupigwa kwa sababu Temeke walikuwa wamefunga penalti nne.


wakati hayo yakiwatokea Mjini Magharibi, Temeke walikuwa wakishangilia kwa nyimbo mbalimbali huku kocha mkuu wa timu hiyo, Shwari Bilanga akitamba kunyakua ubingwa wa michuano hiyo mwaka huu.
"Mjini Magharibi ni timu ya kuogopwa maana ina historia nzuri kwenye mashindano haya... nia yangu ni kuchukua ubingwa na milango sasa imefunguka, viungo wetu wamecheza vizuri ila tulikuwa na tatizo katika umaliziaji na mabeki," alisema Bilanga.


Aliongeza "tumetengeneza nafasi nyingi lakini hatukuwa na bahati katika dakika 90, ndio maana Mjini Magharibi wanalia kwa sababu walikuwa na kila sababu ya kushinda mechi hii."


Naye nahodha wa Temeke, amewaomba wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuiunga mkono timu yake kwa kuishangila katika mechi ijayo ya nusu fainali ili itinge katika fainali na kunyakua ubingwa wa michuano hiyo ya vijana chini ya umri wa miaka 17.


Mechi hiyo namba 93 ya robo fainali za michuano ya Copa Cocacola kati ya Temeke na Mjini Magharibi ilichezeshwa na refa Sadi Ally akisaidiwa na Ramadha Sadiki na Hamad Saidi (wote waamuzi yosso) kutoka Dar es salaam.


 

No comments:

Post a Comment