Tuesday, July 10, 2012

MIKWARA YA KUPELEKA WANAWAKE WASIOOGA KWA WAZIRI MAGHEMBE YAMLIPA MHE. KESSY WA NKASI

Mhe. Prof. Jumanne Maghembe

Mhe. Kessy
Mikwara aliyotoa jana Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Mhe. Ali Kessi Mohamed kuwa angewapeleka bungeni wanawake wa eneo la Namanyere lililopo jimboni kwake, ambao wamekuwa wakitaabika kwa muda mrefu na kushindwa hata kuoga kutokana na ukosefu wa maji, imeanza kumlipa baada ya serikali kutangaza mpango kabambe wa kumaliza kero hiyo.

Akizungumza bungeni jioni hii wakati akihitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, amesema kuwa serikali imesikia kilio cha Mhe. Kessy na kwamba sasa inatenga Sh. Bilioni 2 za kukamilisha mradi wa maji wa Namnyere anaoamini kuwa utamaliza kero ya maji jimboni humo (Nkasi Kaskazini)

Profesa Maghembe alisema kuwa amezungumza na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na kujadiliana naye kwa kina kuhusu suala hilo ambapo mwishowe, wamekubaliana kuwa fedha hizo zitatafutwa na kupelekwa Nkasi.

Waziri Maghembe pia aliahidi kuongozana na Mhe. Kessy kwenda Nkasi ili kuzungumza na wakazi wa huko, wakiwemo akina mama wa Namanyere ili awaeleze namna serikali yao ilivyodhamiria kuwaondolea kero ya maji.

"Kwa sababu hii, namuomba Mhe. Kessy asiwalete hao akina mama bungeni na pia aunge mkono bajeti ya wizara yangu," alisema Prof. Maghembe.

No comments:

Post a Comment