Tuesday, July 31, 2012

MBUNGE ALALAMIKIA ‘AMBULANCE’ ZA BAJAJI

Ambulance ya magurudumu matatu kama hii ndizo alizolalamikia Mbunge wa Nkenge. 

Mhe. Asumpta Mshama (kushoto)

Mbunge jimbo la Nkenge, Mhe. Asumpta Mshama, amelalamikia uwezo mdogo wa ‘ambulance’ za magurudumu matatu na kuihoji serikali kuwa itawasaidiaje akina mama wajawazito ambao wanashindwa kuwahishwa hospitalini kutokana na udhaifu wa vyombo hivyo katika kumudu barabara za jimboni kwake.

Mhe. Asumpta alihoji umadhubuti wa ambulance hizo kwenye barabara mbaya za jimboni kwake wakati wa kupitisha vifungu vya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka ujao wa fedha.

“Maeneo kama ya Nkenge na Minziro bajaji hizi huwa hazifiki… sasa naomba nielezwe kuwa serikali itawasaidiaje akina mama wajawazito wa maeneo kama hayo?” Alihoji Mhe. Asumpta.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alisema kuwa uamuzi wa serikali kusambaza ‘ambulance’ za magurudumu matatu ni kusaidia utoaji wa huduma za afya hasa kwa akina mama wajawazito pindi wanapotakiwa kuwahishwa hospitali kwani ambulance za magari zinauzwa kwa gharama kubwa sana, ambapo gharama za gari moja ni sawa na kununua ambulance za bajaji 10.
“Tutafanya tathmini na kuona namna ya kusaidia watu wa maeneo hayo ambayo ambulance hizi (za bajaji) huwa hazifiki,” alisema Dk. Mwinyi.

No comments:

Post a Comment