Saturday, July 14, 2012

KOCHA ALALAMIKA KUTOSIKILIZWA KIPIGO YANGA

Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga wameanza vibaya kampeni za kutetea taji lao la michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya kukumbana na kipigo cha 2-0 kutoka kwa mabingwa wa Burundi, Atletico, katika mechi ambayo wenyeji wangeweza kufungwa hata magoli SITA, shukrani kwa kipa Mghana Yaw Berko, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.


Atletico walitawala mechi nzima tangu kipindi cha kwanza na wachezaji wa Yanga walionekana kushindwa kucheza kama timu huku safu yao ya ulinzi ikijichanganya hasa kipindi cha pili baada ya kuingia mchezaji mpya waliyemsajili kutoka Toto African, Ladislaus Mbogo.

Mbogo alipigwa chenga "akalamba sakafu" wakati shujaa wa mabao mawili ya Atletico, Didier Kavumbagu, alipofunga goli la kwanza katika dakika ya 81 na mabeki wa kati waliingia katika lawama tena katika dakika ya nne ya majeruhi pale walipopanda mbele ya eneo lao na kumlazimisha kipa Berko kutoka akijaribu bila ya mafanikio kumzuia Kavumbagu asifunge goli la pili katika nyavu tupu.


Ushujaa wa Berko uliiepushia Yanga aibu ya pili mfululizo ya vipigo vikubwa katika mechi za kimashindano baada ya mara tatu katika dakika tano za mwisho wa mechi kuwanyima wageni magoli zaidi. Katika mechi yao ya mwisho ya kimashindano, Yanga walilala 5-0 kutoka kwa mahasimu wao Simba katika mechi ya kufungia msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.


Ikiwa imejaza wachezaji wapya, Yanga ilionekana kukosa mtu wa kuiongoza kubadilisha mchezo na kuwafanya wachezaji kwa muda mwingi kuhaha kuusaka mpira "kwa tochi".


Baada ya mechi, kocha mpya Mbelgiji Tom Saintfiet, ambaye amekumbana na kipigo katika mechi yake ya kwanza ya kimashindano, alilalamikia wachezaji kutofuata maelekezo yake.

"Hata nilipowaambia wabadilike, wachezaji waliamua kuendelea kucheza mpira wa pasi fupi fupi badala ya kucheza wa moja kwa moja wa kwenda mbele. Hauwezi kushinda hata siku moja kama utacheza bila kumsikiliza kocha. Kulikuwa na udhaifu katika eneo la ulinzi wa kati," alisema kocha huyo huku akionyesha kufadhaishwa na namna timu yake ilivyocheza.


"Hakuna visingizio, wenzetu wamecheza vizuri sana. Ni mabingwa wa nyumbani kwao Burundi na walicheza mechi ya kujiandaa dhidi ya timu ya Congo na wakashinda 4-1 na tulifahamu hilo kabla. Nawapongeza, ni timu nzuri sana, walikuwa ni matawi ya juu dhidi yetu leo," alisema Saintfiet.


Kocha wa Atletico, alisema kipindi cha kwanza walicheza kwa kujilinda zaidi na walikuwa wakiwasoma wapinzani wao. "Wakati wa mapumziko niliwaeleza kuwa udhaifu wa Yanga ni mabeki wa kati na hawana kasi hivyo wacheze pasi fupi fupi na kushambulia kupitia katikati," alisema kocha huyo.

No comments:

Post a Comment