Thursday, July 12, 2012

KASEJA ANG'ARA KATIKA PENATI DHIDI YA AZAM NA KUIPA SIMBA UBINGWA KOMBE LA URAFIKI


*RAGE AFANYIWA UPASUAJI INDIA

Umenikosa hiyo...mchezaji wa Simba akikwepa kwanja usiku huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Picha: Khalfani Said

Felix Sunzu wa Simba (katikati) akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao la kwanza.  
Picha: Khalfani Said

Nahodha Juma Kaseja akibebwa juu juu baada ya kudaka penati mbili za Azam na kuisaidia Simba kuibuka na ushindi usiku huu na hivyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Urafiki. Picha: Khalfani Said

Kaseja akishangilia baada ya kukabidhiwa kombe la ubingwa wa Urafiki Cup. Picha: Khalfani Said
Na Mwandishi Wetu
KIPA Juma Kaseja alidaka penati mbili na kuisaidia klabu yake ya Simba kutwaa ubingwa wa Kombe la Urafiki baada ya kushinda kwa penati 3-1 katika mechi yao ya fainali iliyoamuliwa kwa ‘matuta’ kufuatia sare ya 2-2 katika muda wa kawaida kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo usiku.

Mwinyi Kazimoto, Amir Maftah na Kigi Makassy ndio waliofunga penati za Simba huku Haruna Moshi ‘Boban’ akikosa baada ya penati yake kugonga ‘besela’, wakati aliyefunga bao la Azam akiwa ni Khamis Mcha pekee. 

Kaseja ambaye pia ni nahodha wa Simba, alidaka kiufundi penati za Waziri na Mwaipopo huku Himid Mao akipaisha na hivyo kuipa Simba ubingwa wa michuano hiyo ikiwa ni siku moja tu kabla ya kuanza kampeni yao ya kuwania taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).

Katika dakika 90 za kwanza, Simba mabao yao kupitia Felix Sunzu na Mwinyi Kazimoto aliyefunga kwa penati huku mabao ya Azam yakiwekwa wavuni na Mcha Khamis na John Bocco.

Kwa ushindi huo, Simba walizawadiwa kombe na fedha taslim Sh. milioni 10 wakati Azam walizawadiwa Sh. milioni 5.

RAGE APASULIWA INDIA
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amefanyiwa upasuaji wa mgongo katika Hospitalia ya Apolo nchini India na sasa anaendelea vizuri.

Akizungumza kutokea India jana, Rage alisema kwamba madaktari 10 ndio waliomfanyia upasuaji huo, wanne wakiwa ni mabingwa na anashukuru kuwa sasa anajisikia mzima.

“Nashukuru kwa dua za Watanzania, hivi sasa naendelea vizuri,” alisema Rage.

Vikosi:
Simba: Juma Kaseja, Shomari Kapombe/Haruna Shamte (dk.45), Amir Maftah, Mungusa, Juma Nyoso, Mussa Mudde/Haruna Moshi ‘Boban, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Salim Kinje/Uhuru Selemani(dk.61), Felix Sunzu/Kigi Makassy (dk.74) na Abdallah Juma/Danny Mrwanda (dk.45).

Azam: Deogratias Munishi, Ibrahim Shikanda, Waziri Juma, Said Moradi, Joseph Owino/Agrey Morris (dk.45), Ibrahim Mwaipopo, Kipre Bolou/Jabir Aziz (dk.66), Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Kipre Tchetche/John Bocco (dk.45), George Odhiambo na Khamis Mcha.

No comments:

Post a Comment