Saturday, July 7, 2012

CHAMELEONE: BIFU NA MDOGO WANGU LINAKUZWA

*Atamani kufanya wimbo na Ali Kiba

Dk. Jose Chameleone (katikati) akiwa na mdogo wake Weasel TV (kushoto) na Radio (kulia) enzi hizo kabla ya kuanza kuripotiwa kwa bifu baina ya wasanii hao.


NYOTA wa muziki wa Uganda, Dr. Jose Chameleone, amesema bifu linalozungumzwa kwenye vyombo vya habari baina yake na mdogo wake, Weasel, ambaye pia ni mwanamuziki maarufu Afrika Mashariki, linakuzwa na wanahabari.

"Yule ni mdogo wangu baba mmoja, mama mmoja. Hatuwezi kuwa na bifu. Tukiwa na bifu mama yetu atatuangalia vipi?" alisema.

Muimbaji huyo wa wimbo unaotamba wa 'Valu Valu' amesema wakati akihojiwa katika kituo cha radio cha CLOUDS FM muda mfupi uliopita kwamba hata hivyo wao ni binadamu hivyo kutofautiana ni jambo la kawaida.

"Sisi ni binadamu pia. Kutofautiana ni kawaida. Mnatofautiana mnapatana, lakini hatuwezi kuwa na bifu," alisema muimbaji huyo.

Alipoulizwa kama bifu linalotangazwa baina yao ilikuwa ni mbinu ya mdogo wake kutafuta "njia ya kutokea" kisanii, Chameleone ambaye siku hizi anajiita "Dokta" alisema kilichotokea kilikuwa ni "real" na hapakuwa na maigizo.

Na alipoelezwa kwamba baada ya kushirikiana na mdogo wake huyo katika wimbo wa "Bomboclat" siku nyingi zilizopita anaweza kufanya naye tena wimbo kuthibitisha kwamba hawana bifu, alisema hilo linawezekana.

"Yeye yuko bize, ana pesa zake, ana mambo yake na mimi niko bize na mambo yangu, lakini wakati ukifika tutafanya wimbo wa pamoja," alisema.

Alipoulizwa na msikilizaji ni msanii gani anayempasua kichwa nchini Uganda, Chameleone alisema "ni Chameleone" kabla ya kuongeza "sio kwamba wasanii wazuri hawapo, ila wanatoka unawategemea lakini wanapotea baada ya mwaka mmoja tu."

Ali Kiba ...ebwana jamaa anakukubali, mcheki kabla hajaondoka

Dk. Jose pia alielezea kuvutiwa na msanii wa Tanzania, Ali Kiba, akisema anatamani kufanya naye ngoma ya ushirikiano.

 "Sijawahi kukutana naye uso kwa uso, lakini natamani kufanya naye kazi," alisema Dk. Jose.  

Mganda huyo atapanda jukwaani saa tatu usiku katika Tamasha la Usiku wa Matumaini kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ambapo ataonyeshana kazi na nyota wa Bongo, Diamond Platinumz.

Kutakuwa na matukio mengi katika Tamasha la Matumaini leo ambapo pia waigizaji Wema Sepetu na Jacqueline Wolper watapanda jukwaani kuzidunda kabla ya Francis Cheka kuzichapa na Japhet Kaseba.

Wabunge mashabiki wa klabu ya Simba watacheza mechi ya soka dhidi ya wabunge wanaoishabikia Yanga.

No comments:

Post a Comment