Monday, July 30, 2012

ANDY CARROLL HATIMAYE ATUA WEST HAM KWA MKOPO

Andy Carroll
Andy Carroll


LONDON, Uingereza
WEST Ham United imeafikiana na Liverpool kulipa paundi milioni 2 kwa ajili ya kumsajili kwa mkopo Andy Carroll.

Mkopo huo wa msimu mmoja kwa mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya England una kipengele cha kumsajili kwa mkataba wa kudumu Carroll kwa paundi milioni 17, kama West Ham itabaki katika Ligi Kuu ya England.

Hata hivyo, inaaminika kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 hataki kuondoka jumla Liverpool.

Liverpool ilikataa ofa kutoka Newcastle ya kumsajili tena mshambuliaji huyo, baada ya kumnunua kutoka katika klabu hiyo kwa ada iliyoweka rekodi ya klabu ya paundi milioni 35 Januari 2011.

Carroll, ambaye alifunga goli moja kwa timu yake ya taifa katika fainali za Euro 2012, ameshindwa kuonyesha makali yake tangu uhamisho wake uliogharimu fedha nyingi, ambapo amefunga magoli 11 katika mechi 56 alizocheza.

Alionekana kuwa mchezaji asiye na nafasi Anfield kufuatia kutua kwa kocha wa zamani wa Swansea, Brendan Rodgers na kusajiliwa kwa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Italia, Fabio Borini kutoka Roma.

Rodgers alisema Liverpool haitasikiliza ofa ya kuchukuliwa kwa mkopo kwa mchezaji huyo, lakini kocha huyo raia wa Ireland Kaskazini anaonekana anajiandaa kumruhusu Carroll (23), kwenda kufanya kazi na kocha wa zamani wa Newcastle, Sam Allardyce klabuni West Ham.

Carroll pia alihusishwa na mipango ya kutua katika klabu ya Italia ya AC Milan.

Mshambuliaji huyo alianza maisha yake ya soka klabuni Newcastle, akacheza kwa mkopo wa msimu mmoja Preston, kabla ya kurejea klabuni hapo na kuwa mfungaji aliyeongoza katika msimu wa 2009-10 wakati Newcastle ikirejea kwenye Ligi Kuu ya England.

Carroll alipata medali ya ushindi wa Kombe la Carling akiwa na Liverpool msimu uliopita, akianza katika kikosi cha kwanza cha timu yake kwenye Uwanja wa Wembley katika fainali dhidi ya Cardiff City.

No comments:

Post a Comment