Friday, June 15, 2012

Mchezaji wa klabu ya soka ya Simba na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Shomari Kapombe (kushoto) akipokea tuzo ya Mchezaji Chipukizi wakati wa Tamasha la Tuzo za Wanamichezo Bora nchini lililoandaliwa na TASWA juzi usiku. 

TUZO TASWA YAMLIZA KAPOMBE


Na Amur Hassan
MSHINDI wa tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Tanzania, Shomari Kapombe alilia kama mtoto wakati akihojiwa na wanahabari kuhusu tuzo hiyo kubwa aliyoipata akiwa ameichezea Simba kwa msimu wake wa kwanza tu tangu asajiliwe.
Kapombe ambaye pia alishinda zawadi ya Mchezaji Chipukizi, aliondoka ukumbini Diamond Jubilee zilikofanyika tuzo hizo juzi usiku akiwa 'amekunja' Sh. milioni 13, moja ikiwa imetokana taji dogo aliloshinda na Sh. milioni 12 kwa taji kubwa la jumla.
Mchezaji huyo kiraka ambaye licha ya umri mdogo wa miaka 19, alikuwa nguzo muhimu katika klabu ya Simba msimu uliomalizika ambapo alicheza takriban kila namba kikosini mwao ukiacha nafasi ya kipa na mshambuliaji wa kati na kuisaidia klabu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania kutoka kwa mahasimu wao Yanga.
Baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Kapombe alizungukwa na wanahabari pembeni ya jukwaa la tuzo hizo zinazoandaliwa kila mwaka na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) kwa ajili ya kutaka kujua ameipokeaje zawadi hiyo.
Kapombe ambaye alimshukuru Mungu, familia yake, waandaaji wa tuzo, wachezaji wenzake, viongozi na mashabiki wa Simba akisema haamini kama ameshinda tuzo, alimwaga machozi baada ya kumkumbuka aliyekuwa kiungo wao katika kampeni za ubingwa, Patrick Mutesa Mafisango, aliyefariki kwa ajali ya gari akitokea katika klabu ya usiku hivi karibuni.
Yosso huyo ambaye wikiendi iliyopita aliifungia timu ya taifa ya Tanzania, Stars Stars, goli la kusawazisha katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Gambia wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014, hakuweza tena kuzungumza tangu hapo, huku akiendelea kulia, alirejea kwenye kiti alichokuwa amekaa pamoja na nyota wenzake wa Stars na kocha wao Kim Poulsen hadi wenzake walipomtoa nje ya ukumbi kwa ajili ya kwenda kujiandaa na safari ya Stars ya Msumbiji asubuhi yake.
Aggrey Morris wa Azam alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora, Emmanuel Okwi alishinda tuzo ya mchezaji bora wa kigeni anayetamba nchini na Mbwana Samata alishinda tuzo ya mchezaji bora Mtanzania anayetamba nje. Mwanahamisi Omari 'Gaucho' wa Twiga Stars alishinda tuzo ya mwanasoka bora wa kike.

No comments:

Post a Comment