Thursday, June 21, 2012


HISPANIA WAMHOFIA RIBERY


 
Ribery akijifua na wenzake leo kabla ya kutoka nje akichechemea
 GNIEWINO, Poland
Kiwango cha Alvaro Arbeloa katika fainali za Euro 2012 kimekuwa kikipondwa nyumbani kwao Hispania na Ufaransa wanatarajiwa kumtumia winga wao hatari, Franck Ribery kutumia udhaifu huo wakati watakapovaana Jumamosi katika mechi yao ya robo fainali.

Mara kadhaa Arbeloa alionekana akiyumba katika nafasi yake ya beki wa kulia katika mechi zote tatu za Hispania za Kundi C mjini Gdansk, hasa alipokumbana na washambuliaji machahari kama Ribery ambao wana kasi na ujanja mwingi, hivyo kuibua wito wa kumtaka kocha Vicente del Bosque amkalishe benchi na nafasi yake acheze Juanfran.

Akicheza kwa namna ya kushambulia zaidi na pia akiwa ngangari katika kuzuia, Juanfran anaelezewa vilevile kuwa ni mzuri pia katika kupiga krosi ‘kali’ zaidi ya Arbeloa, jambo ambalo linaweza kumlazimisha Ribery ashuke ili asaidie ulinzi.

Hata hivyo, Del Bosque haelekei kuwa tayari kucheza kamari kwa mchezaji ambaye ndio kwanza alianza kuichezea Hispania mwishoni mwa Mei na hivyo ni wazi kwamba ataendelea kumuamini Arbeloa, ambaye anajiandaa kucheza mechi ya 39 kwa timu yake ya taifa mjini Donetsk Jumamosi.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari katika kambi ya Hispania mjini Gniewino, kaskazini mwa Poland leo, Juanfran aliunga mkono Arbeloa acheze, lakini akaongeza kwamba naye yuko tayari kucheza wakati wowote atakapohitajika.

"Yeye ni mchezaji mwenzagu na nitamtetea mpaka kufa," beki huyo mwenye miaka 27 alisema.

"Hivi sasa kocha anamuamini Alvaro na mimi ninaheshimu sana maamuzi yake," aliongeza.
"Ninamuamini na pia kikosi timu nzima inamuamini. Kwa mtazamo wangu amecheza vizuri katika hatua ya makundi na pia alikuwa na msimu mzuri sana kwenye klabu yake ya Real Madrid."

 RIBERY ‘NOMA’

Juanfran
Arbeloa
Yeyote atakayepewa kazi ya kumchunga Ribery, mabingwa wa Dunia na Ulaya watamtegemea sana wakati wakiwania nafasi ya kucheza nusu fainali dhidi ya Ureno au Jamhuri ya Czech, alisema Juanfran.

Ribery alitoka nje ya uwanja wao wa mazoezi huku akichechemea jana Jumatano kutokana na uvimbe , lakini msemaji wa timu alisema kwamba atakuwa ‘fiti’ wakati Ufaransa ikijaribu kulinda rekodi yao ya kutowahi kufungwa na Hispania katika mechi za mashindano, ikishinda tano na kupata sare moja.

"Kila wakati (Ribery) anaweza kutengeneza nafasi ya kufunga kwa ajili yake mwenyewe au kutoa pasi ya goli," Juanfran alisema.
"Ni miongoni mwa wachezaji nyota wa Ufaransa na tunachotaka ni kuona kuwa hana siku nzuri na pia kuona kwamba tunamudu kumzuia yeye na wahsambuliaji wenzake."

No comments:

Post a Comment