Wednesday, June 27, 2012

SILVA: INIESTA MKALI KULIKO RONALDO, MESSI
Bila watu watatu hazuiliki...Hapa Iniesta akijaribu kuwachambua kama karanga wachezaji wa Ufaransa katika Euro 2012.
Kweli Iniesta noma! Hapa machachari yake yanamfanya alindwe vikali ni wachezaji walioshiba wa Italia katika mechi yao ya hatua ya makundi ya fainali za Euro 2012.


Kiungo mchezeshaji wa Hispania, David Silva amesema atampa nafasi ya kwanza mchezaji mwenzake wa kimataifa wa Hispania, Andres Iniesta kuwa mchezaji bora wa Dunia kabla ya nyota wawili wanaochukuliwa kuwa ndio bora zaidi katika miaka ya hivi karibuni, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Hispania wanacheza dhidi ya Uren leo usiku katika mechi yao ya nusu fainali ya Euro 2012, huku Silva na Iniesta wakitarajiwa kuvaana uso kwa uso na Ronaldo, ambaye ameng’ara katika michuano hiyo tangu ‘alipochemsha’ katika mechi mbili za ufunguzi za hatua ya makundi dhidi ya Ujerumani na Denmark.

Iniesta pia amekuwa akionyesha kiwango cha juu tangu kuanza kwa michuano hiyo na hadi sasa ana wastani wa kutoa pasi zinazowafikia wenzake kwa asilimia 91, lakini ni mchango wake wa jumla katika kikosi cha Hispania ndio unaomfanya Silva ammiminie sifa, akigusia ni kwa namna gani amekuwa mhimili wa kikosi chao kinachofundishwa na kocha Vicente del Bosque.

“Waandishi wa habari kila mara wamekuwa wakiniuliza kuhusu  Messi na Ronaldo na nani kati yao ni bora zaidi, lakini kitu kimoja kwangu kiko wazi kabisa," Silva aliwaambia waandishi wa habari.

“Kwangu mimi, No.1 kwa ubora ni Andres Iniesta kwa sababu ni mchezaji mwenzangu katika kikosi cha Hispania na ninaweza kuona kwamba ana uwezo wa kufanya vitu adimu uwanjani. Andres ni mchawi awapo na mpira na pia ni mtu poa, mchezaji nyota kikosini.

“Siwajui kiundani Ronaldo wala Messi, lakini Andres ni mchezaji nyota na pia ni mtu poa. Muhimu sana kikosini.

“Ureno wana timu nzuri na wanacheza soka safi. Wameonyesha vilevile kwamba wao si Ronaldo tu. Sisi hatujapania mechi hii kwa sababu tu ya kucheza dhidi ya Ronaldo... tuko tayari kucheza dhidi ya timu ya Ureno.“

No comments:

Post a Comment