Wednesday, June 20, 2012

MKWASA AKIRI STORI ZA USAGAJI TWIGA STARS


Mkwasa (kushoto) akiwa kazini katika mechi mojawapo ya Twiga Stars kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. (Picha: Kwa hisani ya freebongo.blogspot.com)  

KOCHA Boniface Mkwasa aliyetangaza kujiuzulu katika timu ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars, amefunguka leo na kusema kuwa ni kweli kulikuwa na tetesi kwamba baadhi ya wachezaji wa Twiga walikuwa wakijihusisha na vitendo vya usagaji.


Kutokana na hali hiyo, kocha huyo akaongeza kuwa yeye na wenzake wa benchi la ufundi walichukua hatua kali za kukomesha mambo hayo.


Akizungumza leo asubuhi wakati wa mahojiano yake kwenye luninga ya Stars TV, Mkwasa alisema kuwa licha ya kusikia tuhuma hizo, yeye hakuwahi kuvishuhudia hata siku moja.


Akaongeza kuwa hayo ni mambo binafsi na kwamba yeye na wenzake walichofanya ni kusisitiza kuhusu nidhamu na kwamba, mara zote walichukua hatua kali dhidi ya watuhumiwa wa tabia hizo na nyingine zinazokiuka maadili ya kambi, ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wahusika kikosini.


"Ni kweli... mimi nimewahi kusikia taarifa hizo," alisema Mkwasa wakati akijibu swali la mtangazaji aliyekuwa akiongoza mjadala kuhusu timu za Twiga na kaka zao (Taifa Stars), ambazo zote zilitolewa hivi karibuni katika hatua za awali za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Twiga waliondolewa na Ethiopia kwa jumla ya mabao 3-1 huku Taifa Stars wakichapwa kwa penati 7-6 kwenye mechi yao ya ugenini dhidi ya Msumbiji kufuatia sare yao ya awali ya mabao 2-2.


Mkwasa aliongeza kuwa yeye na wenzake walipambana vilivyo kukomesha vitendo vinavyokiuka maadili kwa wachezaji wa Twiga ikiwemo kwa baadhi yao kupenda kujifananisha na wanaume, hasa kwa uvaaji wa mitindo ya 'masela' maarufu 'kata K' na pia mitindo ya unyoaji.


Kocha huyo alisema kuwa wachezaji wa sasa wa Twiga wana nidhamu nzuri na kwamba tuhuma nyingi mbaya kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho hazipo tena.


Juzi, Mkwasa ambaye pia ni kocha wa klabu ya Ruvu Shooting inayoshiriki Ligi Kuu ya Bara, alitangaza kubwaga manyanga baada ya Twiga kuondolewa na Ethiopia na kushindwa kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wanawake zitakazofanyika Novemba nchini Equatorial Guinea.

No comments:

Post a Comment