Thursday, June 28, 2012

ALBA ASAJILIWA BARCA KUTOKA VALENCIA

Jordi Alba (kulia) wa Hispania akimng'ang'ania Nani wa Ureno wakati mechi yao ya nusu fainali ya UEFA Euro 2012 kwenye Uwanja wa Donbass Arena Juni 27, 2012 mjini Donetsk, Ukraine.
MADRID, Hispania
BARCELONA wameimarisha safu yao ya ulinzi kwa kumpata mrithi wa Eric Abidal baada ya kuafikiana kumsajili beki wa kushoto wa Valencia na timu ya taifa ya Hispania, Jordi Alba (23), kwa mkataba wa miaka mitano, klabu hiyo ya La Liga ilisema jana.

Uhamisho huo utagharimu euro milioni 14 kutegemea kufuzu vipimo vya afya kwa beki huyo ambaye alisoma katika shule ya soka la Barcelona ya La Masia, klabu hiyo ilisema katika ukurasa wake rasmi wa Twitter.

Baada ya kuonyesha kiwango cha juu akiwa na Valencia, beki huyo mwenye kasi alichichezea timu ya taifa ya Hispania kwa mara ya kwanza dhidi ya Scotland mjini Alicante Oktoba mwaka jana na tangu wakati huo ameifanya namba hiyo ya ulinzi wa kushoto iliyokuwa ikishikiliwa na Joan Capdevila kuwa ni yake ya kudumu akicheza mechi 10 mfululizo.

Akiwa amezaliwa katika mji wa Catalan kama kipa wa Barca, Victor Valdes, alianza soka katika timu ya watoto lakini alitemwa na kujiunga na klabu ya ligi ya mkoa ya UE Cornella kabla ya Valencia kumnasa akiwa na umri wa miaka 17 kwa ada ya uhamisho ya euro 6,000.

Akitawala kwenye wingi, Alba hutumia kasi yake ya ajabu kupanda mbele akiwapita wapinzani wake na kupiga krosi za hatari na amekuwa tishio kubwa kwa wapinzani wa Hispania katika fainali za Euro 2012 wakati wakipigania kutetea taji lao.

Alichangia katika moja ya matukio bora ya michuano hiyo katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Ufaransa katika robo fainali wakati alipopanda mbele na kupiga krosi iliyomkuta Xabi Alonso aliyefunga kwa kichwa goli la kwanza la Hispania.

No comments:

Post a Comment