Saturday, August 24, 2013

USAJILI WA WARUNDI WA SIMBA WAKWAMA, JAVU NAYE AKWAMA YANGA

Tambwe Amisi akibeba kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) wakati akiwa na Vital'O jijini Darfur hivi karibuni. 

KLABU ya Simba haitaweza kuwatumia nyota wake wote watano wa kigeni katika mechi yao ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora kutokana na kukosa vibali vya uhamisho wa kimataifa ITC au vibali vya kufanyia kazi nchini, wakati pia Hussein Javu hataweza kuichezea Yanga dhidi ya Ashanti leo kwa kuwa bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Mtibwa Sugar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo, straika Amisi Tambwe na beki Gilbert John Kaze kutoka Vital'O ya Burundi hawataweza kuichezea Simba kwa vile hawajapata ITC kutoka Burundi na hawana vibali vya kufanya kazi nchini, wakati pia kipa Abel right Dhaila hana kibali cha kufanya kazi nchini, Joseph Owino tayari ITC yake imepatikana lakini hana kibali cha kufanya kazi nchini na ni lazima Simba kwanza imfanyie uhamisho straika Betram Arcadi Mwombeki kutoka Pamba SC.

Vilevile Simba inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji wawili iliyowasajili katika kikosi chake cha U20. Wachezaji hao ni Twaha Shekue Ibrahim 'Messi' kutoka Coastal Union 20 na Adeyun Saleh Seif (Oljoro JKT U20).

Yanga inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Rajabu Zahir Mohamed kutoka Mtibwa Sugar U20 wakati Hussein Omari Javu bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Mtibwa Sugar huku kukiwa hakuna vielelezo vyovyote kutoka kwa mchezaji mwenyewe, Mtibwa Sugar au Yanga kama mkataba huo ulivunjwa au umenunulia na klabu anayotaka kuchezea msimu huu.

Wachezaji waliosajiliwa kutoka nje ambao ITC zimefika na pia wana vibali vya kufanya kazi nchini ni Crispine Odula Wadenya kutoka Bandari ya Kenya na Yayo Wasajja Fred Lutimba kutoka URA ya Uganda waliojiunga na timu ya Coastal Union. Pia Mtanzania Hamis Thabit Nyige aliyejiunga na Yanga kutoka Ureno naye tayari na ITC.

Kwa ujumla, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imezuia usajili wa wachezaji 37 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kutokana na usajili wao kuwa na kasoro.

Klabu husika zimetakiwa kurekebisha kasoro hizo kabla ya kuanza kuwatumia wachezaji hao kwenye mechi za VPL ambazo zinaanza leo (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja mbalimbali nchini.

JKT Ruvu Stars inatakiwa kuwafanyia uhamisho (transfer) wachezaji Salum Machaku Salum aliyekuwa Polisi Morogoro na Emmanuel Leonard Swita (Toto Africans). Mgambo Shooting inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Mohamed Hussein Neto (Toto Africans), Kulwa Said Manzi (Polisi Morogoro) na Mohamed Ally Samata (African Lyon).

Pia Salum Aziz Gilla anaonekana bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Coastal Union huku kukiwa hakuna vielelezo vyovyote kutoka kwa mchezaji mwenyewe, Coastal Union au Mgambo Shooting kama ulivunjwa au umenunulia na klabu anayotaka kuchezea msimu huu.

Tanzania Prisons inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji James Mjinja Magafu kutoka Toto Africans na Six Ally Mwasekaga (Majimaji). Nayo Coastal Union inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Kenneth Abeid Masumbuko kutoka Polisi Morogoro.

Kagera Sugar inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Suleiman Kibuta Rajab (Toto Africans), Godfrey Innocent Wambura (Abajalo), Eric Mulera Muliro (Toto Africans), Adam Juma Kingwande (African Lyon) na Peter Gideon Mutabuzi (Toto Africans).

Pia Kagera Sugar imepata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Kitagenda Hamis Bukenya, lakini bado hana kibali cha kufanyia kazi nchini (work permit).

Kwa upande wa Ruvu Shooting inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Abdul Juma Seif (African Lyon), Lambele Jerome Reuben (Ashanti United), Juma Seif Dion (African Lyon) na Cosmas Ader Lewis (African Lyon).

Oljoro JKT inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Tizzo Charles Chomba kutoka Polisi Morogoro, lakini imekataliwa kumsajili mchezaji Damas Mussa Kugesha wa Mlale JKT kwa kigezo kuwa ni askari na amehamishiwa Arusha kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi. Kama Oljoro JKT inamtaka mchezaji huyo ni lazima ifuate taratibu za usajili kwa kumfanyia uhamisho kutoka Mlale JKT.

Nayo Mtibwa Sugar inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Ally Shomari Sharrif (Polisi Morogoro), Salim Hassan Mbonde (Oljoro JKT U20) na Hassan Salum Mbande iliyemsajili kwenye kikosi chake cha U20 akitokea Oljoro JKT U20.

Ashanti United haiwezi kumtumia Said Maulid Kalikula aliyekuwa akicheza Angola kwa vile hajapata ITC. Nayo Rhino Rangers inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Ally Ahmad Mwanyiro (Mwadui FC), Laban David Kambole (Toto Africans) na Musa Boaz Chibwabwa (Villa Squad).

Kwa mujibu wa kanuni, wachezaji wote wa ridhaa (wa madaraja ya chini ikiwemo Daraja la Kwanza) wanatakiwa kufanyiwa uhamisho (transfer) kwa klabu husika kujaza fomu za uhamisho na kulipia ada Chama cha Mpira wa Miguu cha Wilaya, Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa na TFF.

Pia TFF inakumbusha kuwa wachezaji wanaotajwa kuwa wamesajiliwa kama wachezaji huru (free agent) ni lazima waoneshwe kama huko walipokuwa mikataba imekwisha au la.

No comments:

Post a Comment