Friday, August 16, 2013

COCA COLA YATOA MIPIRA 100, FULANA 800


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeishukuru kampuni ya Coca Cola kwa kukabidhi fulana 800 na mipira 100 kwa ajili ya ngazi ya mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 ngazi ya mikoa yanayoanza Septemba Mosi mwaka huu.

Coca Cola ndiyo inayodhamini mashindano hayo yaliyoanzia ngazi ya wilaya ambapo mwaka huu yatachezwa kwa kanda na baadaye fainali itakayochezwa kuanzia Septemba 7-14 mwaka huu jijini Dar es Salaam ikishirikisha mikoa 16 itakayokuwa imefanya vizuri katika ngazi ya kanda.

Kila mkoa utapata fulana 25 na mipira mitatu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya timu zao kwa ajili ya michuano hiyo ngazi ya kanda itakayomazika Septemba 6 mwaka huu.

Kanda hizo ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Singida inaunda Kanda ya Arusha.

Zanzibar itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja wakati Kanda ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara, Temeke na mkoa mmoja wa Unguja.

Kanda ya Mbeya inaundwa na Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma wakati Dodoma, Morogoro, Pwani na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.

Mwanza itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za Arusha timu mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro itaingiza timu mbili.

Wakati huo huo, semina ya makocha 32 wa timu za mikoa zitakazoshiriki michuano ya U15 FIFA Copa Coca-Cola iliyokuwa ikiendeshwa na mkufunzi Govinder Thondoo kutoka Mauritius inafungwa leo (Agosti 16 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment