Wednesday, July 10, 2013

STARS WATAKIWA KUTOKATA TAMAA

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, akikabidhi zawadi maalumu kwa mchezaji wa timu ya taifa, Nadir Haroub (Cannavaro), jijini Dar es Salaam jana wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na Kilimanjaro Premium Lager ambao ni wadhamini wa Taifa Stars. Zawadi kama hizo zilikabidhiwa kwa wachezaji wote na benchi la ufundi.

Wadhamini wa timu ya taifa (Taifa Stars), Kilimanjaro Premium Lager, wamewataka Watanzania kutokata tamaa licha ya Taifa Stars kutofuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia Brazil mwakani kwani timu imeonesha uwezo wa hali ya juu mpaka sasa.

Ombi hilo lilitolewa na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe wakati alipowaandalia Taifa Stars chakula cha jioni katika hoteli ya Tansoma ikiwa ni utaratibu wa wadhamini hao kama njia ya kuwakaribisha wachezaji kambini.

Alisema bado kuna mashindano mengine kama CHAN na AFCON ambayo wana imani Taifa Stars itafuzu na kwuweka historia.

Aliwaasa wachezaji kuhakikisha wanashinda mechi dhidi ya Uganda haa nyumbani na pia watakapoenda Uganda baadaye mwezi huu katika mechi ya kuwania kufuzu mashindano ya CHAN mwakani nchini Afrika Kusini.

“Tumeshindwa kufuzu kwenda Brazil basi twende Afrika Kusini mwakani,” alisema Kavishe.

Alisema wao kama wadhamini wamefarajika kuona jinsi timu ya taifa imepiga hatua tangu waanze kuidhamini mwaka jana.

“Klabu vya  Simba na Yanga zilikuwa na nguvu sana na moja ya dhamira zetu kama wadhamini ilikuwa ni kuinua kiwango cha Taifa Stars na kufanya Watanzania warudishe imani kwa timu yao na sote ni mashuhuda kwani katika mechi ya kwanza kabisa mwaka jana uwanja ulikuwa na watu 10,000 tu lakini katika mechi dhidi ya Ivory Coast hivi majuzi uwanja ulijaa kabisa,” alisema.

Meneja huyo pia alitumia nafasi hiyo kutoa zawadi maalumu kwa wachezaji hao ambazo ni pamoja na DVD zilizorekodiwa maelezo (profiles) za kila mchezaji, kazi ambayo ilifanywa kitaalamu kwa udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager.

Wachezaji wataweza kutumia kazi hizi kwenye mitandao ili waweze kujulikana vizuri ndani na nje ya nchi.

“Tulisema tunaijenga timu na timu inajengwa na wachezaji na ndio maana tumeamua kufanya kazi kama hizi ambazo zitapandisha hadhi ya wachezaji,” alisema huku akitoa wito kwa klabu kutosita kuwaruhusu wachezaji wakati wanaitwa kurekodi kazi kama hizo.

Kwa upande wake, kocha wa timu ya taifa, Kim Poulsen aliwashukuru wadhamini na kusema, “Kwa kweli mmekuwa zaidi ya wadhamini maana ushirikiano mlioonesha ni wa hali ya juu.”

Alisema wachezaji wana ari kubwa sana kwani matunzo wanayopata sasa hivi ni ya hali ya juu na wote wanalenga kupata mafanikio.

Taifa Stars iko kambini kuanzia Julai 4 mwaka huu ikijiandaa na mechi dhidi ya Uganda Jumamosi hii na mechi ya marudiano itapigwa wiki mbili zijazo Mjini Kampala ili kuwania kufuzu katika mashindano ya CHAN.

No comments:

Post a Comment