Monday, July 22, 2013

SIMBA, YANGA KUKIPIGA OKTOBA 20

Haruna Chanongo (kushoto) wa Simba akipeana shughuli na David Luhende wa Yanga wakati wa mechi yao iliyopita ya kufungia msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini dar es Salaam. yanga ilishinda 2-0. Timu hizo mbili kubwa nchini zitakutana msimu huu Oktoba 20. 

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2013/2014 inaanza kutimua vumbi Agosti 24 mwaka huu kwa timu zote 14 kuwa viwanjani katika miji saba tofauti, huku miamba ya soka nchini Simba na Yanga ikicheza mechi yao ya kwanza usiku wa Oktoba 20 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, kabla ya ligi hiyo kuanza kutakuwa na mechi ya kufungua msimu (Ngao ya Jamii- Community Shield) kati ya bingwa mtetezi Yanga na Makamu bingwa Azam itakayochezwa Agosti 17 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi za Agosti 14 mwaka huu zitakuwa kati ya Yanga na Ashanti United (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Mtibwa Sugar na Azam (Uwanja wa Manungu, Morogoro), na JKT Oljoro na Coastal Union (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).

Nyingine ni Mgambo Shooting na JKT Ruvu (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Rhino Rangers na Simba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City na Kagera Sugar (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya), na Ruvu Shooting na Tanzania Prisons (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani).

Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Novemba 3 mwaka huu wakati wa pili utamailizika Aprili 27 mwakani.

No comments:

Post a Comment